ZOEZI LA UBORESHAJI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA LAANZA RASMI WILAYANI SIKONGE
Afisa Mwandikishaji jimbo la Sikonge, Martha Luleka atoa mafunzo kwa Maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata leo katika ukumbi wa Chuo cha Ufundi (FDC). "...nawapongeza kwanza kwa kupata nafasi hii muhimu pia nawaomba muwe karibu na wananchi wakati wa zoezi hili ili kumfanya aweze kutoa taarifa zilizosahihi za mpiga Kura na kuziingiza katika mfumo." Alisema Afisa Mwandikishaji Jimbo.
Mafunzo yalianza kwa maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata kwa kula kiapo cha kujitoa kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kiapo cha kutunza siri mbele ya Hakimu, Mheshimiwa Amando Nyami.
Mafunzo haya yanayoratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni muendelezo wa mafunzo kwa wote watakaoshiriki katika zoezi zima la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga kura, ambapo tarehe 4 na 5 ya Mwezi Oktoba 2019 yalifanyika mafunzo ngazi ya Mkoa.
Afisa mwandikishaji Msaidizi jimbo la Sikonge, bwana Edward Mwamotela kwa niaba ya Afisa Mwandikishaji jimbo alifungua mafunzo haya kwa kusoma hotuba ya ufunguzi ya mafunzo na kuwakaribisha maafisa kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Cecilia Kisaka na Steven Nyoka ambao wameshiriki katika kuratibu mafunzo haya ngazi ya Jimbo.
Pia, bwana Mwamotela aliwasisitiza maafisa waandikishaji wasaidizi ngazi ya Kata kushiriki kikamilifu katika mafunzo haya ili wakatekeleze zoezi hili kwa umakini na ufanisi, pia alisisitiza katika utunzaji wa vifaa vyote vitakavyohusika katika zoezi hili.
Lengo la mafunzo haya ni kuhakikisha zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura linafanikiwa kwa kiwango kikubwa ili kuwa na taarifa sahihi za wapiga Kura.
Katika zoezi hili, wataandikishwa wapiga kura wapya, kwa maana ambao hawakupata nafasi ya kujiandikisha mwaka 2015, ambao wametimiza miaka 18 au watakao kuwa na umri wa miaka 18 ifikapo 2020, pia watapatiwa vitambulisho vipya kwa waliopoteza au kuharibika vitambulisho vya awali na watafutwa kwenye Daftari wale ambao wamepoteza sifa za kuwa wapiga Kura.
Aidha, mafunzo ya siku mbili yatafanyika pia kwa Waandishi Wasaidizi na _BVR Kit Operator_ tarehe 11 na 12 Oktoba 2019, ambao watahusika moja kwa moja katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la wapiga kura ambalo litafanyiaka kwa muda wa wiki moja kuanzia tarehe 14 hadi 20 Oktoba 2019.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa