Na, Edigar Nkilabo – Sikonge DC
Wasimamizi wa vituo na Wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura Jimbo la Sikonge wametakiwa kutoa kipaumbele kwa kundi la watu wenye mahitaji maalumu wakati wa zoezi la kupiga kura tarehe 29 Oktoba, 2025.
Hayo yamesemwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge Mwl.Benjamin Mshandete wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wasimamizi wa vituo na Wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura.
“Natoa wito kwenu nyote siku ya uchaguzi mtoe kipaumbele kwa watu wenye mahitaji maalumu kama wajawazito, wenye ulemavu, wazee na wanaonyonyesha ili na wao wapate fursa ya kuchagua viongozi wanaowataka na hili si takwa langu mimi bali ni utekelezaji wa taratibu, kanuni na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi”
“Aidha kagueni vifaa vyote mtakavyokabidhiwa na kujiridhisha kama kila kitu kipo kwa ajili ya siku ya uchaguzi, sio aje mpiga kura siku hiyo mtu aanze kulalamika kunakitu hakipo”aliongeza Mwl.Mshandete.
Naye Afisa Uchaguzi Ndg.Geofrey Hamis ametoa rai kwa Wasimamizi wa vituo na Wasimamizi wasaidizi kuzingatia mafunzo wanayopatiwa na maelekezo yote ya Tume Huru ya Taiifa ya Uchaguzi ili waweze kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.
“Sikilizeni kwa makini ambapo hamjaelewa ulizeni maswali ili ukitoka hapa uwe vizuri kwa ajili ya kutimiza majukumu ya INEC.Jingine ni kuviishi viapo vyenu kwa kuzingatia sheria, kanuni ,taratibu na miongozo ya tume yaani hatutarajii kuona mtu anakiuka maelekezo ya tume”alisema .
Mafunzo hayo yamefanyika katika kumbi mbalimbali ikiwemo ukumbi wa Mwanambuya, ukumbi wa Elimu maalumu na Shule ya sekondari Kamagi ambapo Wasimamizi wa vituo na Wasimamizi wasaidizi wa vituo vya kupigia kura wapatao 1353 wamehudhuria mafunzo hayo tayari kwenda kusimamia uchaguzi mkuu Oktoba 29, mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa