Na Edigar Nkilabo – Sikonge DC.
Makarani waongozaji wapiga kura wapatao 551 kutoka Jimbo la Sikonge wamekula viapo mbele ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge, Ndg. Benjamin Mshandete wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya Uchaguzi Mkuu ambapo amewataka kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Akifungua Mafunzo hayo katika Ukumbi wa Mwanambuya kwa Makarani waongozaji wapiga kura Jimbo la Sikonge, Mshandete amewasisitiza Makarani hao kuviheshimu viapo walivyoapa na kufanya kazi kwa niaba ya INEC ambayo imewateua na kuwapa vitabu vya miongozo ya utendaji kazi.
“Hapa nyote mmeteuliwa na INEC sio kwa bahati mbaya bali ni kwa mujibu wa sheria za Tume, sasa nendeni mkafanye yale mnayoelekezwa na Tume kwa mujibu wa Katiba yetu, sheria ,kanuni na miongozo yake”
“Pia nitoe wito kwenu Makalani hakikisheni mnawasaidia wenye mahitaji maalumu pindi watakapofika katika vituo vya kupigia kura ili waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowahitaji”aliongeza Ndg. Mshandete.
Kwa upandwe wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge, Nico Kayange wakati akitoa mafunzo kwa Makarani amewataka kutunza vifaa vyote watakavyokabidhiwa kwa ajili ya zoezi la Uchaguzi Mkuu.
“Tunzeni vifaa vyote ili zoezi liende vizuri lakini pia hakikisheni mnabandika mabango yote ya Uchaguzi kama Tume inavyoelekeza ili wananchi waone na kusoma mapema ili siku ya Uchaguzi wasihangaike”alisema.
Mafunzo hayo ya siku moja yamehudhuriwa na Makarani waongozaji wapiga kura kutoka kata 20 za Wilaya ya Sikonge.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa