Kamati ya Fedha, Uongozi, na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, imetembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kipindi cha robo ya kwanza cha mwaka wa fedha 2024/2025, kuanzia Julai hadi Septemba.
Ziara hiyo imelenga kutathmini utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ukarabati inayolenga kuboresha huduma za elimu na afya kwa wananchi wa Sikonge. Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa manne, mabweni mawili, matundu kumi ya vyoo, na nyumba ya mwalimu mbili kwa moja katika Shule ya Sekondari Sikonge, kwa jumla ya Tsh. 508,000,000, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 30.
Kamati hiyo imekagua pia ukarabati wa majengo sita katika Hospitali ya Wilaya ya Sikonge, Mlogolo, kwa Tsh. 100,000,000, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 50. Miradi mingine ni ujenzi wa shule mpya ya amali ya mkoa inayojengwa katika kijiji cha Mlogolo kwa Tsh. 1,600,000,000, utekelezaji umefikia asilimia 30; umaliziaji wa ofisi ya kata ya Mkolye kwa Tsh. 10,000,000, ambapo ujenzi umefikia asilimia 80; ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Buriani kwa Tsh. 60,000,000, ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100; na ukamilishaji wa zahanati ya Ibaya kwa Tsh. 50,000,000, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 70.
Kwa jumla, miradi sita iliyokaguliwa ina thamani ya Tsh. 2,328,000,000, na inatarajia kuboresha huduma za elimu na afya katika wilaya ya Sikonge. Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango imeeleza kuridhishwa kwake na utekelezaji wa miradi hii, ambayo inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii. Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Mhe. Lwamabano, ametoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi za miradi ya maendeleo kwa wilaya ya Sikonge.
Mhe. Lwamabano amempongeza pia Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Sikonge Ndg. Selemani Pandawe kwa usimamizi mzuri wa miradi hii na kueleza kuwa thamani ya fedha zinazotumika inaonekana wazi kupitia maendeleo haya. Miradi hii ni ishara ya dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuleta maendeleo endelevu na kuboresha huduma za kijamii, hususan katika sekta za elimu na afya, ambazo ni nguzo muhimu katika kuinua ustawi wa wananchi wa Sikonge na Tanzania kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa