Na, Edigar Nkilabo – SikongeDC
Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari Bi.Kalista Maina ametoa rai kwa wazazi na walezi wilayani Sikonge kuungana kwa pamoja na kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha Wanafunzi wa kike kusoma masomo ya Sayansi ili kuwa na wastani mzuri wa Wanasayansi wa kike nchini ambao wataendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia katika kuihudumia jamii na taifa kwa ujumla.
Bi.Maina ametoa rai hiyo katika Ukumbi wa Samia Hall uliyopo shule ya Sekondari Kamagi wakati wa mafunzo ya kuwezesha mwanaume na mwanamke kushiriki kikamilifu kukuza elimu ya Sayansi kwa Wanafunzi wa kike.
“Rai yangu kwa wazazi na walezi tuungane kwa pamoja kupiga vita ujinga kwa watoto wetu wa kike, mtoto wa kike akitiwa moyo akifundishwa na kthaminiwa anaweza kufanya vizuri kwenye masmo ya sayansi hivyo kwa pamoja tupinge hii hali ili tuwe na Wanasayansi wazuri watakaojenga familia bora na kulitumikia taifa kwa weledi”alisema.
Naye Mratibu wa mafunzo hayo Mwl.Benjamin Mshandete amewataka Maafisa Elimu,Wenyeviti wa Bodi za shule na Wakuu wa shule kwenda kuhamasisha watoto wa kike kupenda masomo ya Sayansi na kuachana na dhana ya kuwa Masomo ya Sayansi ni magumu na kuwaachia Wanafunzi wa kiume.
“Wakuu wa shule na Walimu wa Sayansi fanyeni ziara ya kubadilishana ubunifu kati ya vilabu vya Sayansi kwa pamoja mpeane mbinu za kuwawezesha Wanafunzi wa kike kufanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi” aliongeza Mwl.Mshandete.
Kwa upande wake Afisa Tarafa Bi.Faraja Hebel akizungmza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Wilaya amesema Walimu wakitoka kwenye mafunzo wakawaulize Wanafunzi wa kike wanapata changamoto gani wanaposoma masomo ya Sayansi na majibu yao yatasaidia Walimu kuja na mbinu nzuri za kuwafundisha watoto.
Aidha Bi.Faraja amewashauri Walimu wa Sayansi kuwa na utaratibu wa kuwaalika Wanawake waliosoma Sayansi na kufanikiwa ili wawe wanafika shuleni na kuongea na Wanafunzi wa kike hii itawaongezea hamasa na kusoma kwa bidii.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF na kuhudhuriwa na Wenyeviti wa Bodi za shule,Wakuu wa shule na Walimun wa Sayansi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa