Na, Edigar Nkilabo SikongeDC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mwl.Selemani Pandawe amewataka Wakuu wa Divisheni na Vitengo kutimiza wajibu wao kwa kutafuta namna sahihi ya kuwasaidia wananchi kupitia sekta zao ili kutimiza lengo la serikali la kutoa huduma bora na endelevu kwa wananchi.
Akizungumza katika Ukumbi wa Halmashauri wakati wa kikao cha Kamati ya lishe ya Halmashauri, Mwl. Pandawe amesema ni wajibu wa watendaji kutafuta majawabu ya changamaoto za Wananchi likiwemo suala la upatikanaji wa chakula shuleni wakati wote.
“Tunahitaji kushirikiana wakati wa kutimiza majukumu yetu, lazima tuje na mkakati wa kuhakikisha watoto wote wanapata chakula wanapokuwa shuleni maana kitendo cha baadhi ya watoto kutokula chakula kinaweza kutengeneza matabaka hivyo tuwabaini na kupata jawabu sahihi la changamoto hiyo”alisema.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amewapongeza wataalamu wa kilimo kwa kuzingatia ushauri wa kamati ya lishe ya Halmashauri kwa kupeleka mashamba darasa kwa taasisi za serikali hasa shule ambapo pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Halmashauri zitawanufaisha wanafunzi pindi watakaposimamiwa vyema katika kilimo na kuzalisha kwa tija”aliongeza Mwl.Pandawe.
Kwa upande wake Afisa lishe wa Wilaya Raymond Joseph amesema kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026, kumekuwa na kuongezeka kwa hali ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi wawapo shuleni.
“Ukiangalia takwimu kwa robo hii idadi ya wanafunzi wanaopata chakula shuleni imeongezeka kutoka 95.6% kwa robo ya nne 2024/2025 na kuweza kufikia 96.23% kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025/2026 na hata utekelezaji wa siku ya afya na lishe ya kijiji imetekelezwa kwa 100% ” alisema Bw.Joseph.
Naye Mratibu wa wilaya wa Mradi wa BRIGHT kutoka shirika la Nutrition International kwa kushirikiana na Shirika la Engeder health na TAWLA Bi.Khadija Kalipeni ametoa wito kwa kamati ya lishe ya Halmashauri kuwatumia wadau mbalimbali kuchangia chakula cha watoto wawapo shuleni badala ya kupambana na wazazi peke yao.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, jumla ya kaya 11,846 zenye watoto chini ya miaka 5 na wajawazito zimetembelewa na kupewa elimu ya lishe kupitia wahudumu wa Afya ngazi ya jamii kwa kipindi cha Julai hadi septemba, 2025.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa