NAIBU WAZIRI ATOA AGIZO WADAIWA SUGU WA ARDHI KUFIKISHWA MAHAKAMANI
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula atoa maagizo kwa Mwanasheria na Afisa Ardhi Wilayani Sikonge kuhakikisha wanaandaa taratibu za kuwapeleka mahakamani wadaiwa sugu wa Ardhi Wilayani humo.
Hatua hiyo inafuatia baada ya wadaiwa hao kupewa notisi ya kulipa kodi lakini wameendelea kukaidi na mpaka sasa hawajalipa fedha hizo zinazodaiwa..
Mabula ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake Wilayani Sikonge ya kufuatilia madeni na kukagua shughuli mbalimbali za sekta ya Ardhi ikiwemo kutembelea masijala ya Ardhi iliyopo ndani ya Halmashauri ya Sikonge.
Mhe. Angelina Mabula akikagua masijala ya Ardhi zilizopo ofisi za Halmashauri ya Sikonge mapema alipokuwa ziara yake Wilayani hapa.
Alitaja baadhi ya wadaiwa sugu kuwa ni Kampuni ya TLTC, WETCO, TRA na mengine mengi, alionesha kusikitishwa na Shirika la Umma TRA kuwa miongoni mwa wadaiwa sugu wakati ilitakiwa kuwa mstari wa mbele katika kulipa kodi.
Alisema kuwa fedha hizo ni muhimu zikakusanywa na kuwasilishwa serikalini ili zisaidie shughuli mbalimbali za maendeleo kama vile ujenzi wa Reli ya kisasa, mradi wa umeme ujenzi wa vituo vya afya na hospitali kwani mpango wa serikali kwa sasa ni kutumia mapato ya ndani ikiwemo kodi katika kutekeleza miradi hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa watendaji wanaohusika katika ukusanyaji kodi kufanya haraka kwani baadhi ya wadaiwa sugu ikiwemo kampuni ya TLTC wamemaliza shughuli na wanategemea kuondoka nchini.
Wakati huo huo Mabula aliziagiza Halmashauri Mkoani Tabora kutumia wasomi kutoka chuo cha Ardhi kilichopo Mkoani hapo kupima maeneo na mashamba ya Wananchi ili yaweze kuingizwa katika makazi bora sambamba na kuwapatia wananchi uchumi.
Jambo hilo lilipokelewa na Mkurugenzi wa Halmashauri Martha Luleka pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Peter Nzalalila na kuahidi kuzingati maagizo hayo.
Sanjari na mazungumzo hayo pia Mhe. Mabula alipata wasaa wa kutembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda Wilayani hapa, eneo hilo lenye ukubwa wa Ekari 8.5 limeshapimwa tayari kwa ujenzi wa viwanda. Jambo hilo lilipongezwa na Mabula kwani wamezingatia kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda.
Mhe. angelina Mabula akipata maelezo toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri (pichani) wakati alipotembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya Viwanda Wilayani Sikonge
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa