Na Edigar Nkilabo,- Sikonge DC
Kutokana na mgogoro wa Wavuvi na Mwekezaji wa pori la hifadhi ya wanyamapori Uyumbu, Wajumbe wa Kamati ya kutatua mgogoro kutoka wilaya za Sikonge na Urambo wamekutana wilayani Urambo kujadili na kupata jawabu la kudumu la mgogoro huo.
Kikao hicho kimeongozwa na Wakuu wa wilaya za Urambo chini ya Mhe.Dkt.Khamis Mkanachi na Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga , wajumbe wa kamati hiyo kutoka Halmashauri zote mbili za Urambo na Sikonge pamoja na baadhi ya Wataalamu wa maliasili kutoka wilaya hizo.
Kamati hiyo imejadiliana na kuhimiza kuwa ni lazima shughuli za uvuvi kufanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu ili kuwezesha uvuvi endelevu wenye manufaa kwa wavuvi na utunzaji wa mazingira kwa kuzuia matumizi ya zana haramu za uvuvi zinazoathiri uvuvi wenye tija na endelevu.
Aidha kamati hiyo imeagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi wa rasilimali maji katika mto Walla zihakikishe zinafanya doria kwa kuzingatia sheria , kanuni na uadilifu ili kuzuia matumizi ya zana haramu za uvuvi pamoja na kutenga eneo kwa ajili ya mazalia ya samaki katika mto Walla na kuhimiza shughuli za uvuvi kufanyika kwa msimu mmoja ambao ni kuanzia mwezi Januari hadi Mei ili kuwa na uvuvi endelevu.
Sambamba na hayo, kamati imeagiza idadi ya wavuvi wanaopewa vibali izingatie uwezo wa eneo linalotumika kwa shughuli za uvuvi ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima na mwekezaji wa hifadhi ya Wanyamapori Uyumbu pamoja na taasisi zingine za uhifadhi.Pia Wataalamu wamesisitizwa kuendelea kutoa elimu ya uvuvi bora ili kuendeleza ikolojia ya eneo hilo.
Kwa kuhitimisha kamati hiyo imeagiza maafisa wa doria kuandaa mpango kazi na kuwa waadilifu wakati wa kutekeleza majukumu yao na kutoa taarifa ya utekelezaji kwa Makatibu Tawala wa wilaya za Urambo na Sikonge.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa