Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Fadhil Rajabu Maganya, amefanya ziara ya kikazi wilayani Sikonge kwa lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuzungumza na wanachama wa chama hicho.
Akiwa katika ziara hiyo, Ndugu Maganya amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa Chuo cha VETA Sikonge, ambacho kinajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 3, na ujenzi huo umefikia asilimia 35. Alitembelea pia mradi wa bwawa la maji la Igumila, lililopo kijiji cha Kapumpa, ambalo linajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.1, na ujenzi huo umefikia asilimia 85. Bwawa hili linatarajiwa kuhudumia vijiji sita na kunufaisha watu 45,000.
Pia, Ndugu Maganya amekagua ujenzi wa vyumba 8 vya madarasa na matundu 12 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Kiwere, mradi ulioigharimu shilingi milioni 234, ambao umefikia hatua ya ukamilifu.
Katika mkutano wake na wananchi wa Kata ya Kitunda,Kijiji cha Lukula, Mwenyekiti Maganya amesisitiza umuhimu wa kila mtendaji wa serikali kutimiza wajibu wake ipasavyo, bila kusubiri malalamiko ya wananchi kufikia viongozi wakuu. Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024. “Uchaguzi huu ni huru, na vyama mbalimbali vya siasa vitasimamisha wagombea. Chama Cha Mapinduzi kimeelekeza kuwa wagombea wanaopaswa kusimamishwa ni wale wenye sifa,” alifafanua Ndg. Maganya.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi kuhakikisha maendeleo yanatekelezwa kwa ufanisi na kuwahamasisha wananchi kushiriki Uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa