WANAOKWAMISHA UJENZI KUVUNJIWA MKATABA
Mkurugenzi Mtendaji Bi. Martha Luleka akiambatana na Wakuu wa Idara watembelea ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Sikonge ili kutathimini changamoto mbali mbali zinazokwamisha mradi huo kutoenda na muda.
Wakiwa kwenye jengo la mama na mtoto walibaini upungufu mkubwa wa nguvu kazi ,ambapo idadi ndogo ya watenda kazi ikiwemo mafundi na vibarua ambao walikuwa hawawezi kuendana na kasi iliyotakiwa.
Wakizungumza na fundi msimamizi walitoa ushauri kwa injinia Erasto Apronex Mtewa aliyepewa mkataba wa jengo hilo kuwa ahakikishe ameongeza idadi ya watenda kazi ikiwemo kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati huku akionywa kutotoa visingiziokuwa vifaa vinachelewa.
Akitaja sababu za kuchelewesha kazi Apronex alidai kuwa vifaa vya ujenzi havifiki kwa wakati huku akitaja mawe na matofali kuwa vinamkwamisha ambapo wajumbe walitoa onyo kuwa waache kutoa visingizio kwani vifaa wanavyodai kucheleweshewa bado wanavyo katika eneo lao la ujenzi na vingi vikiwa havijatumika hivyo basi wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha kazi inafanya na kuzingatia ushauri uliotolewa kwa kuufanyia kazi.
Ikumbukwe kuwa siku chache zilizopita Mkurugenzi Bi. Martha alipokuwa akikagua mradi huo alizungumza na bwana Erasto na kutoa maagizo ya kuongeza nguvu kazi ili kukamilisha kazi kwa wakati lakini hadi wajumbe wanafika eneo la mradi bado hali iliendelea kuwa vile vile. Jambo linalodhihilisha kuwa kinachokwamisha kazi hiyo ni fundi mwenyewe na sio swala la vifaa.
Wakitoa maelekezo kwa mainjinia wote waliokabidhiwa mradi wa ujenzi huo, wakuu wa Idara walisema kuwa kila fundi anatakiwa kuwasilisha mpango kazi wake ambao utabainishasiku hatua zote za ujenzi na muda utakaotumika ambapo ndani ya mpango huo ni vyema ukazingatia muda uliopangwa kukamilisha majengo hayo.
Mkurugenzi pamoja na wakuu wakuu wa idara wakisiliza maelekezo kwa fundi kwenye jengo la Madawa.
Sanjari na hayo walisisitizia kuwa injinia yeyote ambaye ataonesha kukwamisha kazi kuendana na muda atachukuliwa hatua ikiwemo kusitishwa kwa mkataba alioingia na Halmashauri ya Sikonge.
Sikonge ni miongoni mwa Wilaya zilizopata pesa kutoka Serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambapo Halmashauri ya Sikonge ikikabidhiwa jumla ya Tsh. Bil 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa majengo saba ya awali na hatua za ujenzi zinaendelea huku baadhi ya majengo yakiwa kwenye hatua nzuri wakati majengo mengine ikiwemo jengo la mapokezi na wodi ya mama na mtoto yakiwa katika hatua za awali.
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA TEHAMA SIKONGE
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa