Na Edigar Nkilabo – SikongeDC
Zoezi la utoaji wa chanjo kwa ng’ombe dhidi ya homa ya mapafu ya ng’ombe na utambuzi wa mifugo, kuku dhidi ya kideri,ndui na mafua ya kuku kwa wilaya ya Sikonge zoezi hili lilianza June 25, 2025 kwa kuchanja kuku na Agosti 6 mwaka huu ng’ombe nao walianza kuchanjwa ambapo hadi kufikia siku ya uzinduzi wa kampeni hii ya chanjo ya mifugo kwa wilaya ya Sikonge tayari kuku zaidi ya laki Nne wameshachanjwa na ng’ombe elfu Hamsini wameshapatiwa chanjo hiyo katika kata 8 kati ya kata 20.
Hayo yamesemwa na Daktari wa Mifugo Wilaya ya Sikonge Dkt.Maulid Rajabu wakaiti akiwasilisha taarifa ya zoezi hilo kwa mgeni rasmi Mhe.Thomas Myinga alipozindua zoezi hilo katika kijiji cha Isongwa kata ya Mkolye.
“Kabla ya zoezi hili kuanza Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tulipita katika kata zote kuamasisha lengo likiwa ni kuwa na uelewa wa pamoja kati ya wafugaji, viongozi wa ngazi ya vitongoji,vijiji na kata pamoja na wataalam kwa ujumla ambapo hadi kufikia tarehe 27/8 jumla ya ng’ombe 51,890 zimechanjwa na ngombe 9976 zimetambuliwa(zimewekewa herein) na takribani kuku 444,599 zimechanjwa hadi sasa zoezi hili limetekelezwa katika kata 8 kati ya 20” alisema Dkt.Maulid Rajabu
Kwa upande wake Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Huduma za Mifugo Kanda ya Magharibi Dkt.Adelina Mkumbukwa anasema mifugo yote iliyopo Wilayani Sikonge itachanjwa hakuna mfugo utakaoachwa kwakuwa serikali imetoa dozi ya kutosha.
“Tumepewa idadi ya dozi 250,000 hivyo mifugo yote itachanjwa na ikitokea imepelea basi utaratibu utafanyika wa kuongeza dozi hiyo lakini tunayo dozi 450,000 ya kuku pamoja na hereni za utambuzi za bure, niwaombe wafugaji wote wa Wilaya ya Sikonge wajitokeze kwa wingi kuchanja mifugo yao”alisema Dkt.Mkumbukwa.
Seif Salum ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge ameishukuru serikali kwa kutoa chanjo ya ng’ombe kwa bei ya ruzuku na chanjo ya kuku ya bure.
“Mwaka jana wafugaji wetu walikuwa wanatoa sh.1000 kuchanja ng’ombe lakini kwa kwa upendo wa serikali ya Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka ruzuku na kuwapunguzia bei wafugaji wetu ili waweze kuchanja mifugo yao”alisema.
Naye mgeni rasmi Mhe.Thomas Myinga akizindua zoezi hilo amesema serikali imeweka mpango wa chanjo kwa kipindi cha miaka 5 (2024-2029) kwaajili ya ustawi wa wafugaji na taifa hivyo wafugaji hawana budi kuchangamkia fursa hiyo.
“Tumechanja kuku wengi ili kuzuia magonjwa hatari ya kuku kama kideri na ndui ambayo yamekuwa yakiwarudisha nyuma wananchi vivyo hivyo kwa ng’ombe tunaendelea kuchanja leo nimezindua lakini zoezi linaendelea hadi mifugo yetu yote ichanjwe , katika hili niwatake viongozi wa serikali ya kijiji na kata mtoe ushirikiano kwa wataalamu ili tuifikie ile adhma iliyokusudiwa na serikali”alisema.
Uzinduzi rasmi wa kampeni ya chanjo ya mifugo na utambuzi wa mifugo kitaifa ulifanyika June 16, mwaka 2025 huko Bariadi mkoani Simiyu na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 200 ukiwa na lengo la kuchanja na kutambua alama za kielektroniki, mifugo milioni 76 katika kipindi cha miaka mitano inatarajiwa kuchanjwa ambapo hadi sasa mifugo milioni 34 tayari imekwisha chanjwa.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa