Na Edigar Nkilabo, NYAHUA - AGOSTI 26, 2025
Wakazi wa Kata ya Nyahua wanaoishi katika kambi ya Luseseko iliyopo katika eneo la hifadhi ya Msitu wa Nyahuambuga wamehimizwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya kijiji kuimarisha usalama na amani ya eneo hilo ikiwemo ulinzi wa mali zao.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga wakati akizungumza na wananchi wa kata hiyo katika mkutano wa hadhara ambapo amesema jukumu la usalama ni la raia wote kwa mujibu wa katiba hivyo wananchi wote hawana budi kuhakikisha eneo lao linakuwa salama.
“Ndugu zangu Askari tulionao ni wasimamizi wa usalama lakini sisi wananchi ndiyo wenye jukumu hilo la kuhakikisha tunakaa mahali salama na mali zetu zinakuwa salama.Shirikianane na viongozi wenu kuwabaini wahalifu na kutoa taarifa zao haraka kabla ya matukio ya kihalifu nawahakikishia mkifanya hivyo basi Nyahua itakuwa salama na Polisi wetu watawashughulikia wahalifu mara moja tu wanapopata taarifa”alisema.
Aidha Mkuu wa Wilaya amesema tayari serikali imetenga eneo na kulipima kwaajili ya kuwahamisha wananchi wote wanaoishi katika hifadhi ya msitu wa Nyahuambuga.
“Kila kitu kinaendelea vizuri taratibu zitakapokamilika basi tutawaondoa kwenye hili eneo la hifadhi lakini waambieni wenzenu wasije mkaongezeka maana tayari wataalamu walishakuja kuhakiki idadi yenu na orodha tunayo kwa atakayeongezeka huyo hatapata kiwanja ataambulia kuwa ndugu mtazamaji” Mhe.Thomas Myinga alisisitiza.
Naye Afisa Misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu(TFS) wilaya ya Sikonge Eliuter E. Kibiki amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za nchi bila shuruti kwakutokufanya shughuli yoyote katika maeneo ya hifadhi na wale wenye vibali vya kulina asali kujikita katika kazi hiyo kwa mujibu wa vibali vyao.
“Hii misitu ni mali ya taifa tunaitunza kwaajili yetu na vizazi vijavyo hivyo tuwe walinzi wa maeneo haya tuishi kwa kuzingatia sheria na taratibu sio vyema kuingia kwenye hifadhi na kufanya shughuli za kilimo na mifugo hakika nawambieni tukikukuta basi sheria itachukua mkondo wake. N hata wale wenye vibali vya kutundika mizinga jueni hiyo misitu si yenu fanyeni kazi hiyo ya kulina asali na kuondoka”alisisitiza.
Kwa upande Kaimu Afisa Ardhi wa Wilaya ndugu Salum Tabu amewatoa wasiwasi wananchi wa Luseseko na kuwahakikishia zoezi la upimaji wa maeneo ya viwanja unaendelea na eneo watakalopelekwa ni zuri kwani limepimwa na kukidhi vigezo vyote vya kitalaamu.
Kata ya Nyahua ni miongoni mwa kata 20 zilizopo Wilayani Sikonge ikiwa na jumla ya vijiji 3 vya Nyahua,Makibo na Nyahuanga.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa