Na Edigar Nkilabo,
Wanafunzi wa mafunzo ya Jeshi la Akiba (Mgambo) wapatao 54, wanaume 40 na wanawake 14 wamehitimu mafunzo ya Jeshi la Akiba huku wengine 10 wakiishia njia kutokana na vitendo mbalimbali vya utovu wa nidhamu na utoro.
Akifunga mafunzo hayo katika uwanja wa TASAF, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga amewapongeza wahitimu wote na kuwasisitiza kuishi kwa kuzingatia viapo vyao kama askari.
"Mmeapa hapa mbele yetu ninategemea muendelee kuwa waadilifu na watiifu kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Amiri Jeshi Mkuu Dkt.Samia Suluhu Hasaan, na mjue ninyi ni askari wa akiba muda wowote mkihitajika muwe tayari"alisema.
Aidha Mhe.Mkuu wa Wilaya amewataka Askari hao wa akiba kwenda kuielimisha na kuihamasisha jamii kushiriki uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, kwa amani na utulivu.
"Mkawe mabalozi wa amani kwa kuishi vyema na raia mkiwaheshimu viongozi na wananchi, mkawaeleze tarehe 29 mwezi wa 10 wakachague viongozi ambao wataamua maisha yenu"alisisitiza.
Kwa upande wake Mkufunzi wa Mfunzo hayo Afande Dotto Matmil amesema wahitimu wamepata mafunzo mbalimbali ambayo yamewajengea ujasiri na utayari wa kukabiliani na adui pamoja na kulitumikia taifa.
"Tumewapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo mafunzo ya ukakamavu,ujanja porini,kusoma ramani,kutumia silaha, mafunzo ya sheria za nchi pamoja na elimu ya kupinga rushwa hivyo tunaamini wameiva wako tayari kulitumikia taifa"
Naye Askari wa Akiba MGM Agness Samwel akisoma risala mbele ya Afande Mgeni rasmi ameomba serikali kuwatazama kwa jicho la tatu na kuwapa kipaumbele katika fursa mbalimbali za ulinzi katika taasisi za umma.
"Tunaomba zinapotokea kazi za ulinzi tufikiriwe sisi migambo kwanza ikiwemo kazi za doria na hata ulinzi katika maeneo ya taasisi, bila kusahau mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) yakitangazwa basi tupate hiyo fursa"alisema.
Mafunzo hayo ya miezi minne yamehitimishwa hii leo kwa sherehe za gwaride, kareti pamoja na kikosi cha kuruka viunzi huku Afande mgeni rasmi akiwatunuku vyeti Askari walioonesha umahiri katika medani.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa