Na Edigar Nkilabo
Kamati ya Wataalamu ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imefanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya elimu na afya inayotekelezwa katika kata za Kitunda na Kiloli, ambapo kamati hiyo imewataka wasimamizi wa mradi wa shule shikizi Kapumpa kuanza mara moja ujenzi wa matundu 4 ya vyoo katikashule hiyo ili watoto zaidi ya 300 waweze kunufaika na uwepo wa madarsa 6 yaliyojengwa na wananchi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) na kugharimu zaidi ya Shilingi milioni 70.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ndugu Selemani Pandawe ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge akizungumza baada ya ukaguzi wa kamati ya Wataalamu alisema ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa tayari umekamilika wenye kusimamia mradi huo watumia fedha ya jimbo waliyopewa kukamilisha matundu ya vyoo ili watoto wapate huduma katika mazingira bora na kuepuka magonjwa ya milipuko.
“Tumeona madarasa tayari yamekamilika Halmashauri tunawapa mbao 280 mchonge madawati muweke , kamilisheni na hivyo vyoo ili watoto waanze kutumia maana hiyo milioni 5 ya mfuko wa jimbo mmeipata muda mrefu kidogo”alisema.
Aliongeza kuwa yapo baadhi ya mapungufu katika madarasa 6 yaliyojengwa wasimamizi wa miradi wafanye marekebisho yote waliyoambiwa na Mhandisi wa Wilaya ndani ya siku 14 kabla ya kuendelea na ujenzi mwingine.
Sambamba na ziara hiyo ya Kata ya Kitunda, kamati hiyo imetembelea miradi ya elimu na afya katika kata ya Kiloli, mosi ziara ikianzia katika mradi wa shule ya Msingi Mwitikio ambapo wajumbe walitoa maoni yao.
“Fedha za vyumba 4 vya madarasa na vyoo matundu 6, zilitolewa mwaka jana mwezi Julai, sasa tunashangaa hadi sasahivi bado mradi haujakamilika na sababu za msingi hazieleweki”walisema baadhi ya Wajumbe.
Naye Mhandisi wa Wilaya Abdulaziz Iddi amesema changamoto kubwa katika mradi huo ni usimamizi wa kusuasua na mafundi wanaojenga kutofuata maelekezo yanayotolewa na Ofisi yake, jambo linalopelekea mradi kutokumalizika kwa wakati.
“ Mwenyekiti mradi huu wa zaidi ya milioni 60 ulitakiwa uwe umeisha lakini unasuasua kutokana na mvutano wa kamati ya ujenzi na uongozi wa shule kwa ujumla , hapa huwa nikija kukagua naacha maelekezo lakini hayafuatwi”alisema.
Aidha katika ukaguzi wa Zahanati ya Ipembe,Kamati imeshauri jengo la Zahanati liboreshwe zaidi ili milioni 60 zilizotengwa ziwezekupelekwa na kumalizia ujenzi huo, huku serikali ya kijiji ikihimizwa kuweka mipaka ya kudumu katika eneo la Zahanati.
“Wekeni mipaka ya kudumu msiache hivihivi maeneo ya zahanati yakavamiwa na kaya za watu ikiwezekana Mtendaji wa Kijiji na serikali yako tafuteni hela kidogo mpate hati ya Kimila.”alisisitiza Katibu Tawala wa Wilaya Ndg.Andrea Ng’hwani.
Katika kata za Kitunda na Kiloli kamati imehitimisha ziara yake kwa kukagua miradi miwili ya elimu na mmoja wa afya ambapo miradi hiyo imegharimu zaidi ya shilingi milioni 200.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa