WALIMU KUWA MSTARI WA MBELE SHUGHULI ZA MAENDELEO
Walimu waaswa kuwa mstari wa mbele na kushirikiana na jamii kwenye shughuli za maendeleo.
Hayo yalisemwa na katibu wa CCM Wilaya ya Sikonge Bi. Magdalena Daniel alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Shirikisho la Walimu ambao ni wananchama wa CCM Wilayani Sikonge alipokaribishwa kutoa salamu za chama kwa wanashirikisho hao waliokuwa na mkutano wa ndani mapema hivi leo ambapo aliwataka walimu kutumia taaluma yao kuinufaisha Nchi sanjari na kujitoa kwa moyo wa uzalendo wanapohitajika katika shughuli za maendeleo.
Mkutano huo pia ulishirikisha viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya akiwemo Mhe. Joseph Kakunda ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Sikonge, Mhe. Peter Nzalalila ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na wajumbe na viongozi wa Shirikisho hilo ngazi ya Wilaya na walifanikiwa kuzungumza na kutoa maoni mbalimbali yenye tija ya kujenga nchi ya Tanzania.
Miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa ilikuwa ni umuhimu wa Nembo ya Taifa ambapo Mhe. Kakunda aliwataka walimu hao ambao ni wanashirikisho kuwafundisha wanafunzi kuijua Nembo ya Taifa na kuilinda kwani ina maana kubwa kwa kila Mtanzania.
Akiongezea hoja hiyo Mhe. Nzalalila aliwataka wanashirikisho kufanya kazi pasipo na majivuno huku akiwahakikishia watumishi wote kuwa Serikali ina mpango mzuri na maslai yao hivyo walimu walio katika shirikisho wawe mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuhakikisha majukumu waliyopangiwa yanafanikiwa kwa kiwango cha juu na huko ndio kukitumikia Chama Cha Mapinduzi kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ambayo pia ililenga kuboresha sekta ya Elimu.
Walimu wa Shirikisho wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wenye uhitaji maalumu wanaosoma shule ya msingi Sikonge Maalum mapema walipotembelea shuleni hapo.
Akipokea maelekezo hayo kwa niaba ya wajumbe Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Wilayani Sikonge, Mfaume Zahoro aliahidi kuyazingatia yote yaliyoagizwa huku akisema kuwa wanafanya kazi vizuri kwa kushirikiana na Ofisi ya Afisa Elimu (W) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Martha Luleka huku akihakikisha kuwa matokeo bora kwa wanafunzi ni jitihada za walimu katika kuunga mkono juhudi za Mhe. John Pombe Magufuli ambaye ameboresha miundombinu ya elimu na kutoa elimu bure kwa wanafunzi.
Awali kabla ya kuanza kwa mkutano huo wanashirikisho pia walishiriki katika usafi wa mazingira, hii ikiwa ni agizo la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sikonge, Martha Luleka aliyewataka watumishi wote pamoja na wananchi kushiriki kuuweka mji wa Sikonge safi. Tayari utaratibu umewekwa wa kufanya usafi wa maeneo yote kila ifikapo siku ya jumamosi na Wakuu wa Idara na Vitengo wamepangiwa maeneo ya kusimamia na kukagua.
Baada ya Mkutano huo pia wanashirikisho walipata nafasi ya kutembelea shule ya Sekondari Kamagi na kushiriki shuguli za umwagaji wa zege, sambamba na kuongea na wanafunzi wa kidato cha tano ambao wamechaguliwa kwa awamu ya kwanza mwaka huu tangu kuanzishwa kwa shule hiyo.
Imeandaliwa na Kitengo cha TEHAMA Sikonge
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa