Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akiwahutubia Wananchi Wilayani Sikonge tarehe 10 Agosti, 2017 katika viwanja vya TASAF. Mhe. Kassim Majaliwa amezungumzia hasa matatizo yanayowakabili wakulima wa tumbaku katika vyama vyao vya ushirika na pia akapiga marufuku msimu ujao wa tumbaku kutumia DOLA katika ununuzi wa tumbaku. Aidha Waziri Mkuu alimpongeza Afisa ushirika Bwa. Emmanuel Hyera kwa kufuatilia matatizo ya wakulima na kuyatatua.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwataka watumishi wa wilaya hiyo, washirikiane na watendaji na madiwani ili kuongeza mapato ya wilaya hiyo badala ya kuwaachia watendaji wa kata peke yao. Jana, mara baada ya kupokea taarifa ya mkoa wa Tabora, Waziri Mkuu alizitaka Halmashauri tano kati ya nane za mkoa huo zitoe maelezo ni kwa nini zimeshindwa kufikisha asilimia 80 ya makusanyo kama ambavyo waliagizwa na Serikali.
“Halmashauri zilizovuka malengo ni tatu tu, Nzega TC, Kaliua na Nzega DC. Nataka taarifa za halmashauri zilizobakia ifikapo Agosti 25, wakijieleza ni kwa nini hawajafikia malengo ya ukusanyaji mapato yaliyowekwa ambayo ni asilimia 80,” alisema
Pia amezitaka Halmashauri zote zihakikishe zinafanyamakusanyo kwa kutumia mfumo wa kielektroniki. “Ukusanyaji wote wa mapato ni lazima ufanyike kwa mfumo wa kielektroniki. Halmashauri ambazo hazijafanya hivyo, zitumie makusanyo ya mwaka jana kununulia mashine za EFD. Hatutaki kuona risiti za kuandika kwa mkono zinatumika,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa mkoa wa Tabora uhakikishe wanapatikana watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika wilaya hiyo ili waweze kusaidiana na watendaji wa halmashauri hiyo kukusanya mapato.
“Hapa Sikonge naambiwa hakuna ofisi za TRA. Lazima tupate maafisa wa TRA katika kila Halmashauri ili watoe elimu na washirikiane na madiwani, watendaji wa vijiji na watumishi wa Halmashauri juu ya ukusanyaji mapato,” alisema.
Imeandaliwa na Kitengo cha TEHAMA, Sikonge
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa