Na. Robert Magaka – Sikonge.
Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Wilaya ya Sikonge Mhe. Simon Chacha ametoa wito kwa Watendaji wa Kata Wilaya ya Sikonge Kwenda kusimamia upatikanaji wa chakula shuleni leo katika kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata na Wilaya katika kipindi cha robo ya pili,Oktoba hadi Desemba 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
Mhe. Chacha ameongeza kuwa ni lazima watendaji kutumia mbinu zote na rasilimali zinazopatikana katika maeneo yao ya kiutendaji kuwezesha upatikanaji wa lishe bora shuleni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Seleman Pandawe ametoa rai kwa wataalam kuhakikisha wanaishirikisha jamii kikamilifu katika suala zima la uchangiaji wa chakula shuleni ili Watoto waendelee kupata lishe bora shuleni.
Naye Afisa Lishe Wilaya ya Sikonge Bi. Veronica Ferdinand amesema katika robo ya pili utoaji wa chakula shuleni ndio kiashiria pekee ambacho kimeonesha udhaifu katika utekelezaji wake katika kata zote za wilaya ya Sikonge.
Aidha Bi. Ferdinand ameongeza kuwa katika robo hii ya pili Oktoba hadi Desemba yapo mambo mazuri yaliyoonekana wazi ikiwemo kupanda kwa kiashiria cha utekelezaji wa siku ya Afya na Lishe ya Kijiji kutoka 71% (Julai hadi Septemba, 2023) hadi kufikia 98% (Oktoba hadi Desemba, 2023). Vile vile jumla ya miche 500 ya kisasa ya miti ya miembe imepandwa katika shule kumi za Msingi katika Wilaya ya Sikonge ikiwa na lengo la kuboresha lishe shuleni.
Akihitimisha kikao hicho Mhe. Chacha amepongeza kwa juhudi zinazoendelea ili kuboresha lishe katika ngazi ya kata na Halmashauri kwa ujumla, imebainika kuwa kati ya viashiria 10 katika kadi alama za lishe ni viwili tu ndio vipo katika rangi ya njano na nane vilivyobaki vipo katika rangi ya kijani ambayo ni kiashiria cha kufanya vizuri katika utekelezaji wa afua za lishe.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa