Mkuu wa Wilaya ya Sikonge,Mhe. Cornel Lucas Magembe ameongoza kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata na wilaya katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge.
Akifungua kikao hicho,Mhe. Magembe amesema mikoa inayozalisha chakula kwa wingi nchini imebainika kuwa jamii zake zinakumbwa na hali ya utapiamlo mkali, hivyo ni muhimu kuendelea kuelimisha jamii nzima juu ya umuhimu wa kuzingatia lishe kwa ustawi wa taifa letu.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Afisa Lishe wilaya ya Sikonge Bi. Veronica Malamsha,utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata na Wilaya kwa robo ya nne kuanzia Aprili hadi Juni 2024 umefanikiwa kwa kiasi kikubwa. Viashiria vingi vya lishe vimefanya vizuri kwa wastani wa asilimia 91.Hii inaonesha kuwa hatua zinazochukuliwa katika kuboresha lishe zimeleta matokeo chanya.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Sikonge, Ndg. Seleman Pandawe amewaagiza watendaji kusimamia muongozo wa serikali katika utoaji wa chakula shuleni.Muongozo huo unaohusisha ushirikiano kati ya mzazi na mwalimu ni muhimu kuuzingatia ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata lishe bora shuleni bila kuleta mvutano na lawama kwa walimu juu usimamizi wa chakula ambacho wazazi wanachangia.
Akifunga kikao hicho Mhe. Magembe ameendelea kusisitiza umuhimu wa kila mtendaji wa serikali kwa nafasi yake kuhakikisha anasimamia vilivyo malengo ambayo serikali imeyaweka ili yafikiwe kwa muda muafaka na kwa ufanisi unaoleta tija katika jamii.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa