SIKONGE YAANDAA MPANGO MKAKATI WA MWAKA 2019/2020 HADI 2023/2024
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imeanza mchakato wa kuandaa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wiki hii kwa kutoa mafunzo kwa wakuu wote wa Idara na Vitengo ili washiriki kikamilifu katika uandaji wa mpango huo kwa kuwa ndio njia itakayoiongoza Halmashauri kwa miaka mitano.
Mafunzo hayo ambayo leo yanahitimishwa yalianza siku ya Jumatatu katika ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) ambapo Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Martha Luleka alifungua rasmi mafunzo hayo na kuwasisitiza wakuu wa Idara na Vitengo kushiriki na kutoa mawazo yao kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata Mpango wenye tija na maendeleo kwa wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aidha, Bi. Martha Luleka alisema, " hakuna shughuli yoyote utakayo itekeleza nje ya Mpango huu kwa muda wa miaka mitano, kila shughuli utakayo leta maombi kwa ajili ya kutekeleza, mimi nitaangalia tu kama ipo kwenye mpango wetu ndipo nitairuhusu na sio vinginevyo". Aliyasema hayo kuweka msisitizo juu ya mafunzo yanayotolewa na muwezeshaji, Dkt. Titus Mwangeni kutoka Chuo cha Mipango Dodoma.
Muwezeshaji alikaribishwa na Mkurugenzi ili kuendelea na mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku tano. "Maandalizi ya mpango mkakati wa taasisi yoyote huwa ni gharama kubwa sana lakini nyie mmepata bahati kubwa sana kufanya zoezi hili kwa gharama ndogo kwa njia alizozitumia Mkurugenzi wenu," alisema muwezeshaji huyo na kusisitiza pia kila Mkuu wa Idara na Kitengo kushiriki kikamilifu bila kukosa hata siku moja katika mafunzo.
Washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wakuu wa Idara na Vitengo wamefurahi sana kupata mafunzo hayo kutoka kwa Muwezeshaji mwenye ujuzi na uzoefu wa kutosha wa kuandaa Mpango Mkakakati. Katika kuchangia mawazo, Mwanasheria wa Halmashauri, Bwana Paschal Kapinga alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa Halmashauri na kama ikiwezekana ni vema washiriki wote tukapatiwa vyeti vya ushiriki wa mafunzo.
Imeandaliwa na Kitengo cha TEHAMA@2019
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa