Na, Anastazia Maguha – Sikonge.
Ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja Kitaifa mwaka huu , Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge imeadhimisha wiki hiyo kwa kumulika huduma mbalimbali zinazotolewa kwa Wananchi huku ikibeba kaulimbiu ya Huduma bora na endelevu kwa kila Mwananchi INAWEZEKANA.
Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kupitia kitengo muhimu cha Afya katika Hospitali ya Wilaya – Mlogolo wameadhimisha wikii ya Huduma kwa mteja kwa kutoa elimu na kuwasihi Wananchi wa wilaya ya Sikonge na waliopo karibu kufika katika Hospitali hiyo kwa ajili ya vipimo na kupatiwa matibabu pindi wanapobainika kuwa na changamoto za kiafya.
“Tumejipanga vizuri tunatoa vipimo vya magonjwa ya Selimundu ( Sickle cell), Homoni (hormones) , huduma ya Mama na Mtoto lakini pia magonjwa yasiyoambukizwa mfano. Presha na Kisukari na huduma za dharula ( emergency) zote zinapatikana hivyo akija mgonjwa atatukuta tuko tayari kumpatia huduma stahiki na atafurahi”alisema Muuguzi, Rose Mgita.
Kwa upande wake Mtaalam wa maabara, Elkana Paul alisema kwasasa serikali imeboresha huduma kwa kununua vifaa vya kisasa ambavyo vimesaidia na kuwezesha huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali.
“Maabara yetu inahudumia wananchi wote wa ndani na nje ya Sikonge, huduma za vipimo tunazotoa ni vipimo vya ini,figo,homoni, mkojo na malaria hivyo wiki hii ya huduma kwa mteja tunawakaribisha wananchi wote kwani mtaji wa kwanza wa mwanadamu ni afya” alisema Elibariki Paul.
Kwingineko, Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji nayo ilianza maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja kwa kuwatembelea wateja na kutoa elimu ya biashara, sheria za ulipaji kodi pamoja na utoaji wa leseni za biashara kidijitali.
Kaimu Mkuu wa Divisheni hiyo, Princelous Hunja alisema lengo lao ni kuhakikisha mfanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge anapata huduma bora na endelevu hasa kipindi hiki cha maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo huduma nyingi zinatolewa kidijitali.
“Wiki hii wateja wetu waitumie kwa kujifunza na kuzifahamu taratibu zote za upatikanaji wa huduma zetu, na sisi tuko tayari kuwahudumia muda wote kama kuna sehemu hawaelewi wasikae kimya waulize maswali tutawapa majawabu sahihi”alisema.
"Tunawakaribisha Wafanyabiashara wote katika Ofisi zetu zilizopo hapa Halmashauri, kwa ajili ya kupata huduma na elimu mbalimbali juu ya ulipaji kodi na kupata leseni Kidigitali,lakini msisite kutoa maoni na ushauri ili kuboresha huduma hizi ili kwa pamoja tuweze kuleta tija na ustawi wa Halmashauri yetu na Taifa kwa ujumla”aliongeza.
Kaulimbiu ni Huduma Bora na Endelevu kwa Kila Mwananchi Inawezekana.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa