Na Linah Rwambali
Zaidi ya Shilingi Milioni mia tano zimetolewa na serikali kwaajili ya kuanzisha kidato cha tano na sita katika shule ya Sekondari Sikonge ikiwa ni juhudi za serikali katika kuboresha huduma ya elimu nchini.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu wa shule Bi Loveness Mwenda shule pesa hizo zilipokelewa mnamo Juni 2024 kwaajili ya mradi wa ujenzi wa mabweni mawili, madarasa mawili, matundu kumi ya vyoo na nyumba ya mwalimu ya mbili kwa moja. .
Mradi huo ulikuja ili kuiwezesha shule kuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita sababu awali shule ilikuwa na kidato cha kwanza hadi cha nne pekee wakati ilipoanza mnamo mwaka 2023.
Bi.Mwenda anasema mradi huo una uwezo wa kuhudumia wanafunzi 180 yaani mabweni mawili, kila moja likiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi themanini wakati kwa upande wa madarasa manne kila moja likiwa na uwezo wa kubeba wanafunzi arobaini.
“Hata sasa wanafunzi 12 wa kidato cha tano wameripoti shuleni hapo wavulana kumi na wasichana wawili” anasema.
“Kwa sasa shule inatoa mchepuko mmoja wa HGE (History, Geography, Economics) ambapo kuna walimu wote wanaohusika na kufundisha masomo hayo yote” anasema.
Akizungumzia umuhimu wa mradi huo Bi. Loveness anasema anashukuru serikali kwa ujenzi wa mabweni, madarasa, nyumba ya mwalimu na matundu kumi ya vyoo maana utamkinga kijana na vishawishi na kupata muda mzuri wa kujisomea.
“Mtaani kuna makundi ya wavuta bangi, vibaka na mengineyo. Mtoto anapokaa mazingira ya bwenini inamlinda dhidi ya hayo yote sababu amezungukwa na wanafunzi wenzake ambao wana nia kama yake yaani kusoma na kufaulu”
“Kwa upande wa wasichana wanaepuka vishawishi vya kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na hatimaye kupata mimba ambazo hupelekea mwanafunzi kushindwa kutimiza ndoto zake” anasema.
Aliongeza kuwa “watoto wanapoletwa hapa wanajikinga dhidi ya hayo yote sababu huwekwa chini ya mfumo mmoja wa kuwaongoza, wanaelekezwa njia ya kupita na kuwekewa sheria kwa atakayeonekana kukiuka mfumo”.
Aidha Bi Loveness anasema kwa upande wa nyumba ya mwalimu itawezesha wanafunzi kupata msaada iwapo changamoto yoyote itajitokeza.
“Mwalimu kuishi ndani ya shule itawezesha wanafunzi kutoa taarifa iwapo kuna tatizo lolote mfano mtoto kuumwa, umeme kukatika na mengineyo.
“Naishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utaleta tija katika sekta ya elimu Wilayani Sikonge na Tanzania kwa ujumla. Hata sasa tumeshapokea wanafunzi 12 wa kidato cha tano ambao walianza kusoma mnamo Mnamo Julai mwaka huu wakiwemo wavulana kumi na wasichana wawili japo mradi una uwezo wa kupokea wanafunzi 160 yaani madarasa manne ambapo kila darasa linachukua wanafunzi arobaini na mabweni mawili, kila bweni lina uwezo wa kubeba wanafunzi themanini.
Mbali na Mwalimu huyo nao baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha tano katika shule hiyo, wameelezea namna wanavyonufaika na mradi huo kwa mfano Justine Richard anasema mabweni ni mazingira stahiki kwao katika kujisomea kwasababu kuna umeme, huduma ambayo inawawesha kujisomea nyakati za usiku.
“Baadhi ya wanafunzi hatuna umeme majumbani kwetu, kuishi shuleni kunatuwezesha kujisomea katika muda wowote tunaohitaji” anasema.
“Unapokua nyumbani unalazimika kujisomea wakati wa mchana tu wakati wengi tunapendelea kujisomea usiku sababu ni muda uliotulia, unaposoma muda huo unaelewa mambo kirahisi sababu ya uwepo wa utulivu katika muda huo.Naishukuru serikali kwasababu wametutengenezea mazingira ambayo yatatuwezesha kupata muda mwingi wa kurejea yale tuliofundishwa darasani kitu ambacho tusingeweza kukipata tukiwa tunajisomea nyumbani” anasema.
Fatma Juma anasema muda ambao angeupoteza katika kusafiri umbali mrefu wakati anaenda na kurudi shuleni sasa atautumia katika kujisomea kwa bidii akiwa bwenini.
“Kuishi bwenini kunaniwezesha kuokoa muda ambao ningeupoteza wakati wa kwenda na kurudi shuleni. Ninategemea kufanya vizuri katika masomo yangu maana kuishi shuleni kunaniwezesha kusoma kwa kadri nitakavohitaji” anasema.
“Najisikia furaha kupata fursa ya kusoma katika shule hii mpya yenye vifaa na walimu wa kutosha jambo ambalo litachangia kutuwezesha wanafunzi kupata matokeo mazuri” anasema.
Naye Nassoro Kulwa anasema kuwa anafurahi kuishi katika shule ya bweni kwa mara ya kwanza na kupata uzoefu wa kuwa karibu na walimu ambao wanaishi katika nyumba ya mwalimu ilyopo jirani nao.
“Ujenzi wa mabweni na nyumba ya mwalimu umetuwezesha kujenga ukaribu wa kielimu na kijamii na walimu wetu sababu tunaishi karibu na nyumba ya mwalimu. Ninapokua najisomea na kushindwa kuelewa mahali fulani, naweza kumfata mwalimu nyumbani kwake na ukaribu huo wa kuulizana changamoto za kielimu huzalisha urafiki kati ya mwalimu na mwanafunzi jambo ambalo humfanya mwanafunzi kuwa huru kumshirikisha mwalimu hata katika changamoto zake zingine za kijamii” anasema.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa