Na, Edigar Nkilabo – Sikonge DC
Kamati ya Wataalamu(CMT) ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (Mwenyekiti) imefanya ziara katika kata mbalimbali na kukagua miradi ishirini (20) ya elimu, afya na vikundi vya mkopo vya Wananwake vinavyonufaika na mkopo wa Halmashauri wa asilimia kumi unaotokana na mapato ya ndani.
Katika ziara hiyo kamati imeridhishwa na kupongeza utekelezwaji wa baadhi ya miradi ya elimu na afya na miradi mingine ikionekana kusuasua kukamilika kutokana na usimamizi mbovu wa waliopewa dhamana ya kusimamia miradi hiyo na msisitizo wa kamati zaidi ukiwa kwenye uundaji wa kamati za mapokezi, manunuzi na ujenzi unaozingatia mwongozo na taratibu za ujenzi wa mfumo wa kuendesha miradi kwa kutumia nguvu kazi na vifaa vya serikali (Force Account).
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo kwa niaba ya Kamati ya Wataalamu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndugu Selemani Pandawe amesema baadhi ya miradi imekwama kutokana na usimamizi mbovu wa wenye miradi hasa pale unapogundua wamekiunka utaratibu wa kuunda kamati za ujenzi,manunuzi na mapokezi.
“Hakikisheni mnazingatia miongozo ya force account haiwezekani Mtendaji wa Kijiji unakuwa Mwenyekiti wa Kamati sasa ukiwa sehemu ya watekelezaji wa mradi ni nani atakayefuatilia maendeleo ya mradi huo na kubaini mapungufu yanayotokea. Mfano hapa Ipole mradi wa matundu 25 ya vyoo umekwama na fedha ipo kutokana na usimamizi mbovu na kamati zenyewe hazieleweki jamani hizi ni fedha za serikali zitumike kwa kufuata utaratibu unaotolewa na serikali”alisema Pandawe.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji amewasimamisha kazi Watumishi wawili ambao ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ipole na Mtendaji wa Kijiji cha Ipole kwa kushindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na kupelekea kukwama kwa mradi wa ujenzi wa matundu 25 ya vyoo wenye thamani ya shilingi milioni Sitini na Nane unaotokana na fedha za SWASH.
Kwaupande wao baadhi ya Wajumbe akiwemo Katibu Tawala wa Wilaya ya Sikonge wamewapongeza wasimamizi wa miradi ambao wamefanya vyema kwa kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyoendana na thamani ya fedha
“Tuwapongeze kwa kusimamia fedha za mradi kwa weledi na uadilifu hata kuukamilisha mradi huu kwa viwango stahiki, sasa watu wa Ipole wakija hapa watakuwa salama kwa kwakuwa taka zote zitachomwa pia watanawa mikono yao na kuwa salama”alisema Katibu Tawala Ndugu Andrea Ng’hwani.
“Kwakweli baadhi ya wasimamizi wa miradi wako vizuri wanajua nini wanafanya na kamati zao za ujenzi zimeundwa kwa kufuata taratibu na miongozo hivyo ninaamini hizi milioni 250 za ujenzi wa kituo cha Afya Kiloleli zitasimamiwa vyema tukija hapa tutakuta mradi unaenda kwa kasi” alisema Seif Salum Mjumbe wa Kamati.
Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Ipole Dkt.Justina Joseph akisoma taarifa ya kichomea taka na kinawia mikono chenye thamani ya shilingi milioni ishirini (20) amesema ujenzi wa kichomea taka utasaidia kuondoa uchafu na kutunza mazingira.
Kwaupande wake Afisa Manunuzi ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Wataalamu wa Halmashauri amewataka wasimamizi wa miradi kufuata utaratibu wa manunuzi kwa kuhakikisha kamati zote zinatimiza wajibu wake na kutunza nyaraka zote.
“Nyaraka zote za manunuzi zitunzwe ili wakaguzi wanapokuja wakute kila kitu kipo sawa na jambo la mwisho nawasisitiza wanakamti mnatimiza wajibu wenu kulingana na jukumu la kamati husika ili kazi ziende msitegeane”alisema Nibwene Mwaikandage Afisa Manunuzi.
Ziara hiyo ya siku mbili imehitimishwa kwa kukagua miradi ishirini inayotekelezwa katika Kata mbalimbali za Halmashauri ya wilaya ya Sikonge, yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni Moja na Milioni Mianne(Bil.1.4)
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa