Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Simon Chacha ametembelea kata ya Nyahua akiambatana na Maafisa toka Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Tabora,Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya Magharibi,Wakala wa Huduma za Misitu Sikonge,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge na wataalam wake,Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya pamoja na viongozi wa Chama Wilaya ya Sikonge.
Katika ziara hiyo Mhe. Chacha ameongea na Wananchi wanaoishi kwenye eneo la hifadhi katika vitongoji vya Luseseko,Manyanya na Kawemimbi.Akiongea katika Mikutano ya hadhara kwenye vitongoji hivyo Mhe. Chacha amewasilisha Salamu za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kwamba kwa busara na utashi wa Mheshimiwa Rais wananchi wote waliovamia eneo la hifadhi hawataondolewa kama ilivyokusudiwa awali bila kupatiwa eneo lingine la kuishi ili kupisha eneo hilo la hifadhi.
Aidha ameongeza kuwa wapo wataalam toka ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Tabora watakao kwenda kushirikiana na viongozi toka kila kitongoji ili kuona na kupima eneo watakalohamia,hivyo wananchi wameombwa kutoa ushirikiano kwa wataalam hao pindi watakapofika kuanza zoezi hilo.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Sikonge Mhe. Anna Chambala amewasihi wananchi wanaoishi eneo la hifadhi kuwa zoezi litakapokamilika la kuwagawia eneo lingine wasijaribu tena kurudi na kuishi kwenye eneo la hifadhi kwani sheria itafuata mkondo wake.
Kwa upande wao wananchi wa vitongoji vya Luseseko,Manyanya na Mawemimbi wamemshukuru sana Mhe. Rais kwa kuwahurumia na kuamuru wapatiwe eneo lingine la kuishi nje ya eneo la hifadhi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa