NDEGE YAANGUKA NA KUUA RUBANI NA ABIRIA WILAYANI SIKONGE
NA EVELINA ODEMBA
WATU wawili raia wa Afrika Kusini wafariki katika ajali ya ndege iliyotokea mapema asubuhi ya leo majira ya saa moja na nusu katika kata ya Igigwa Wilayani Sikonge.
Watu hao waliotambulika kwa majina ya D. Werner mwenye umri wa miaka hamsini na nane 58 pamoja na Werner Fredrick Fronaman mwenye umri wa miaka 36 wote wanamme raia wa Durbun Afrika ya kusini waliokuwa wakisafiri kwa kutumia Ndege yenye namba za usajili 19-ZU-TAF mali ya Afrika Kusini.
Akielezea tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri alisema kuwa marehemu hao waliokuwa wakitokea Entebe Uganda kuelekea Lilongwe Malawi walipata hitirafu ya injini hivyo walilazimika kutua kwa dharura katika uwanja wa ndege wa Tabora hapo jana, kabla ya kuendelea na safari yao asubuhi ya leo ambapo wakiwa angani muda mchache baada ya kuruka walitoa taarifa kwa watu wa anga kuwa injini imezimika ghafla na baada ya hapo hawakuweza kupatikana tena mpaka taarifa za ajali hiyo zilipopatikana.
“Tumepokea kwa masikitiko makubwa tukio hili kwani hawa ndugu zetu ambao walikuwa katika ziara ya kuhamasisha wanafunzi barani Afrika kusomea elimu ya Anga na kwa upande wa Tanzania walitoa elimu hiyo visiwani Zanzbar” alisema
Sambamba na hilo pia alitoa shukurani kwa vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Tabora kwa kushiri vyema kutoa msaada wakati wa tukio hilo huku akiagiza jeshi la Polisi Wilayani Sikonge kuendeleza ulinzi kwenye eneo ilipotokea ajali hiyo mpaka uchunguzi kamili utakapokamilika.
Naye mwenyekiti wa halmashauri ya Sikonge Mhe. Peter Nzalalila alitoa shukurani kwa wananchi wa kata ya Igigwa ambao walishiriki kutoa taarifa kwa Viongozi mbalimbali pamoja na kuwaokoa marehemu katika ajali na kusisitiza kuwa na moyo huo huo wa kiubinadamu waliouonesha.
Mbali na umati mkubwa wa watu waliojitokeza kuwa mashuhuda wa ajali hiyo pia viongozi mbalimbali ngazi ya Wilaya walifika kutoa msaada akiwemo Mbunge wa Jimbo la Sikonge Mhe. Joseph Kakunda, Mkurugenzi wa Halmashauri Martha Luleka pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilayani hapa.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa