Na Edigar Nkilabo
Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi INEC Mhe, Jaji wa Mahakama Kuu Asina A. Omary amefanya ziara Wilayani Sikonge na kukagua mwenendo wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya Pili.
Akizungumza katika ziara hiyo baada ya kutembelea vituo vitatu vya kata za Sikonge na Misheni Mhe.Asina alisema ameridhishwa na huduma wanayopatiwa wananchi wanaofika katika vituo vya kuboresha taarifa katika Daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili.
“Nimeona wapo wanaokuja kujiandikisha kwa mara ya kwanza,wengine wanahama vituo na baadhi yao wanaboresha na kuhakiki taarifa zao wote hawa nimeona wanahudumiwa vizuri na kupata kadi zao kwa wakati, naamini wakati ukifika basi wataenda kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi wanaowataka yaani madiwani, wabunge na Rais”alisema.
Naye Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Sikonge Mwl.Benjamin Mshandete alisema zoezi hili limetoa fursa kwa wakazi wote wa Wilaya ya Sikonge wenye sifa ya kupiga kura kwenda kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika vituo vilivyopo na kupata kadi, jambo ambalo ni la kuishukuru Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuhakikisha kila mtu anapata haki yake.
“Jimbo letu la Sikonge linavituo 35 ambavyo vinapatikana katika kata zote 20 zilizopo Wilayani Sikonge hivyo kila mwananchi aliyepitwa na zoezi hili awamu ya kwanza safari hii amepata huduma, kwakweli tunaishukuru Serikali na INEC kwa kuwezesha zoezi hili kwa uarahisi”amesema.
Aidha Mwl.Mshandete alisema zoezi limeenda kwa amani na utulivu katika vituo vyote 35, ambapo changamoto pekee zilizojitokeza ni pamoja na kunyesha kwa mvua katika baadhi ya kata ambayo ilichangia kuathiri idadi ya wateja kufika vituoni.
Baadhi ya wananchi kutoka katika vituo tofauti tofauti vya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura walipoulizwa juu ya zoezi hilo walisema huduma zilikuwa zinatolewa kwa weledi na haraka huku wengine wakisema kuwa mashine za Biometriki za sasa zimeboreshwa hazichukui muda mrefu kutoa vitambulisho.
“Yaani nimefika tu sijachukua muda mrefu nimepata huduma na vitambulisho vya safari hii havifutiki haraka vinaonekana vizuri, kwakweli nitoe wito kwa wengine ambao hawajapata wawahi vituoni”
Zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya Pili kwa wilaya ya Sikonge na Mkoa wa Tabora kwa ujumla lilianza Mei, Mosi na kufikia tamati tarehe 07, Mei mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa