Na Edigar Nkilabo
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, wilayani Sikonge kumekuwa na shamrashamra mbalimbali ikiwemo kushiriki katika zoezi la usafi na utunzaji wa mazingira ambapo viongozi wa wilaya, watumishi na wananchi wameungana kufanya usafi katika mitaro ya Barabara za mitaa pamoja na maeneo ya soko la Kariakoo na TASAF.
Akiongoza zoezi hilo Katibu Tawala wa Wilaya ya Sikonge Ndg.Andrea Ngh’wani amesema kuungana na kufanya usafi imekuwa njia nzuri ya kuusherehekea muungano wetu pia ni ishara njema ya umoja wetu hivyo tuungane na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na kujenga utamaduni wa kufanya usafi na kutunza mazingira ya umma na yale yanayotuzunguka ili kuwa salama dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayosababishwa na uchafu.
“Zoezi hili la kukutana na kufanya usafi ni ishara ya kuudumisha muungano wetu na jamii ilifanye zoezi hili la usafi kuwa endelevu ili mazingira yawe safi na salama na hapo tutakuwa mbali na magonjwa ya mlipuko” amesema .
Aidha Katibu Tawala amewataka wananchi wa Sikonge kujitokeza kwa wingi kesho tarehe 26/04/2025 kwenye kilele cha sherehe ya miaka 61 ya Muungano, ambazo zitafanyika katika Uwanja wa TASAF kwa kunogeshwa na Bonanza la michezo ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, kuvuta kamba na kufukuza kuku.
Kwaupande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Nico Kayange amesema kazi iliyofanyika leo ya usafi ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za miaka 61 ya Muungano wetu ambao ni tunu na inaacha alama kwa wakazi wa Sikonge ambao wanapaswa kuendeleza zoezi hili hata siku zingine ambazo si za sherehe.
Zoezi la usafi na utunzaji wa mazingira limehusisha wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wilya ya Sikonge, Viongozi na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Watumishi, wananchi pamoja na Wanafunzi wa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Sikonge (FDC).
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa