Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Silaoneka Kigahe (Mb) amezindua leo Kiwanda cha Kati cha Kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki Sikonge.
Akihutubia wananchi waliohudhuria hafla hiyo Mhe. Kigahe ameupongeza Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Sikonge kwa kufanikisha kujenga kiwanda cha Kuchakata na kufungasha mazao ya nyuki kwani ni kielelezo cha maendeleo ya viwanda nchini na tija kwa wafugaji wa nyuki ambao hapo awali walikuwa wakipata tabu ya soko la uhakika la bidhaa zao.
Aidha amebainisha changamoto za wafugaji wa nyuki ikiwepo ukosefu wa soko la uhakika,matumizi ya mizinga isiyo na kiwango inayopunguza uzalishaji wa asali pamoja na uvamizi wa wakulima na wafugaji katika maeneo ya hifadhi ambapo mizinga hutundikwa hivyo kusababisha nyuki kutoweka na hiyo kuleteleza uzalishaji wa asali kuendelea kuwa duni au kukosekana kabisa.
Hata hivyo Mhe. Kigahe amewahakikishia wananchi wa sikonge kuwa mfumo wa stakabadhi ghalani utasaidia sana kukomesha walanguzi wanao nunua asali kwa bei ya chini isiyoleta tija kwa wafugaji.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Dkt. Batilda Salha Burian ametoa wito kwa wafugaji wa nyuki na wananchi kwa ujumla kuifanya biashara ya mazao yatokanayo na nyuki kuwa mahususi kama nchi zingine zinavyofanya ingawaje zinazalisha asali kwa kiasi kidogo kuliko sisi.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Kiwanda hicho ,Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Seleman Pandawe amesema serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakao ingia kwenye hifadhi za misitu bila kufuata utaratibu uliowekwa ili kudhibiti uhalibifu wa mazingira pamoja na kulinda biashara ya ufugaji nyuki ambao unategemea sana mazingira haya ya hifadhini.
Kwa upande wao wananchi wa Sikonge waliojitokeza katika tukio hili muhimu wamesema wanaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kutekeleza maana ya maendeleo kwa vitendo kwa kuwajengea kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki kwani kitazalisha ajira na kuwasaidia wanachi kuuza asali yao kwa bei yenye tija,ombi lao kwa serikali nikuruhisiwa kuingia na pikipiki kwenye hifadhi wakati wa msimu wa kuvuna asali ili irahisishe shughuli za kubeba mazao yao ukilinganisha na jinsi wanavyotumia baiskeli kwa sasa.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa