Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameipongeza Wilaya ya Sikonge kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo. Pongezi hizo amezitoa leo alipokuwa akikagua miradi ya ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Ukanga na madarasa matatu katika Shule ya Msingi Batilda. Miradi hii inajengwa kwa fedha za mapato ya ndani pamoja na fedha kutoka Serikali Kuu, ambapo jumla ya shilingi milioni 120 zimetumika.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Mhe. Gwajima amepongeza uongozi wa wilaya ya Sikonge kwa kufanya kazi kwa umoja na kusikilizana kati ya chama na serikali , jambo ambalo limechochea maendeleo katika wilaya hiyo na kuifanya iendelee mbele bila vikwazo. Amesisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi wa chama na serikali ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa mafanikio.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Lucas Magembe, amemuomba Mhe. Gwajima msaada wa kuimarisha mapambano dhidi ya mila na desturi kandamizi zinazochelewesha maendeleo, hususan katika sekta ya elimu. Mhe. Magembe ametaja mchezo wa Chagulaga, unaoshamiri zaidi katika jamii ya wafugaji wilayani Sikonge, kama moja ya mila inayosababisha ndoa za utotoni na kukatisha masomo ya watoto wa kike, hasa wa jamii ya Kisukuma.
Ziara ya Mhe. Gwajima imehitimishwa kwa kuweka mawe ya msingi katika ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Ukanga na Shule ya Msingi Batilda. Akihutubia wananchi baada ya zoezi hilo, Mhe. Gwajima amewaomba wananchi kuwa mstari wa mbele katika kupinga mila na desturi zinazokwamisha jitihada za serikali za kuwaletea maendeleo. Ametoa wito kwa wanaume mashujaa kuwa mabalozi wema wa mabadiliko, ili kuelimisha jamii kuhusu mila na desturi zinazozuia maendeleo, hususan mchezo wa Chagulaga.
Mhe. Gwajima amewakumbusha wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya mkoa wa Tabora. Kwa mfano, Serikali imetumia jumla ya shilingi trilioni 1.1 kwa mkoa wa Tabora pekee katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa bilioni 186.6 kwa sekta ya elimu, bilioni 37.5 kwa sekta ya afya, bilioni 199.6 kwa sekta ya maji, bilioni 12.3 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za kilimo, na bilioni 302.4 kwa ajili ya sekta ya nishati,bilioni 281.6 kwa ajili ya sekta ya miundombinu ya barabara na shilingi bilioni 52 kwa ajili ya sekta ya umwagiliaji.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa