Baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora limepitia na kupitisha mapendekezo ya makisio ya Bajeti ya shilingi bilioni 37.074 kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Hayo yamejiri katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ambapo wamejadili taarifa mbalimbali pamoja na kupitisha makisio ya bajeti hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya Mpango huo wa Bajeti Mkuu wa Idara ya Mipango na Uratibu wilaya ya Sikonge, Aidan Flument amesema Bajeti hiyo imezingatia maeneo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge ndg.Selemani Pandawe amesema kila mwaka wa fedha wamekuwa na bidii ya kutenga fedha za mapato ya ndani za miradi pamoja na kusimamia fedha za serikali kuu za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya na elimu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Mhe.Rashid Magope amemtaka Mkurugenzi na wataalamu wa Halmashauri kuongeza ufanisi na uadilifu katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia lengo la makusanyo yaliyopangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe.Cornel Magembe amewasisitiza madiwani kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza makusanyo ambayo yatasaidia kusogeza na kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha Mhe.Magembe amewataka wazazi na walezi kupeleka watoto shule wale wanaotakiwa kuanza darasa la awali na msingi pamoja na wale waliofaulu darasa la sab ana kutakiwa kujiunga na elimu ya sekondari kidato cha kwanza.
“Inasikitisha hadi leo kuna watoto mmekaa nao nyumbani badala ya kuwapeleka shule wakasome nimewaagiza watendaji kushirikiana na migambo kuanza kuwakamata wazazi na walezi wasiopeleka watoto shule na hili halikubaliki kwakuwa serikali ya Mama Samia inatumia fedha nyingi kujenga madarasa na kuboresha miundombinu watoto wasome” amesema.
Katika hatua nyingine baadhi ya wajumbe wa baraza wamewashauri Watendaji wa TARURA na RUWASA kushirikiana na madiwani na baadhi ya viongozi wa ngazi za kata na vijiji katika kuapanga maeneo ya kupelekewa miradi ili kuwa na msawazo wa huduma tofauti na sasa baadhi ya maeneo yanapelekewa miradi mingi ili hali yapo maeneo hayana hali inayoathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa