KAMPENI YA FUKUA FUKUA YATUA RASMI SIKONGE
Na Evelina Odemba
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Agrey Mwanri aendesha kampeni ya fukua fukua Wilayani Sikonge ili kuwabaini wahalifu waliojificha Wilayani hapa.
Kampeni hii iliyoanzishwa rasmi Mkoani Tabora na kutangazwa Wilayani hapa kupitia mkutano wa hadhara, ilijikita kushirikisha wananchi katika utekelezaji kwa kuwataka kuandika majina ya wahalifu wanaowatambua na kuyakabidhi kwa Kamanda wa Polisi Wilaya, huku akiwataka kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi mara watakapoona mtu wasiyemfahamu au wanayemtilia mashaka katika maeneo wanayoishi.
Akifafanua kuhusu kampeni hiyo Mhe. Mwanri ambaye aliambatana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji (W), alisema kuwa zoezi hili litasimamiwa na kuratibiwa na jeshi la polisi wakati wa kuendesha msako wa kuwafukua wahalifu kokote walipojificha kwa kuwashirikisha wananchi kwasababu wao ndio wapo katika maeneo hayo na ni rahisi kupata taarifa kwa haraka.
Aidha alitahadharisha kuwa kila msako utakapoendeshwa basi Polisi wawepo ili kutoa muongozo na taratibu kisheria, huku akionya kuwa hatoruhusu wananchi kujiendea wenyewe kuwakamata wahalifu kwa sababu hataki mtu aonewe, kubugudhiwa wala kufanyiwa vitu vya ajabu.
“Kama una habari yeyote muhimu tunakuomba utoe taarifa kwa jeshi letu la Polisi,wao watalifanyia kazi kwa weledi tunajua kuwa wahalifu wote wanaokuja hapa lazima wana mawakala wao mahali hapa, wacha tuitwe wanoko lakini mahali hapa pabaki salama” alisema.“Hatutakubali wahalifu watoke kokote walipotoka na kuona kuwa Tabora ni sehemu pekee wanayoweza kukaa kwa amani huku wakiendelea kutekeleza uhalifu wao” aliongeza huku akisisitiza kuwa watu wote wafanye kazi muda wa kazi na si kushinda kwenye nyumba za starehe muda wa asubuhi.
Akiongea na wananchi baada ya zoezi la kuandika majina ya wahalifu kwa siri kufanyika kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Barnabas Mwakarukwa aliwataka wale wote walioandikwa majina yao kujisalimisha kituo Kikuu cha polisi kilicho karibu naye haraka iwezekanavyo kabla hawajasakwa kokote walipo.“Tuna mtaji mkubwa sana wa wananchi ambao sio wahalifu, wahalifu ni wachache na mtandao wao unafahamika, kwani wanatoka miongoni mwa jamii” alisema.
Naye mkuu wa wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri alisema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu Wilayani hapa kwani Serikali imejipanga vizuri kiutekelezaji. Hivyo wananchi wawe na amani katika utekelezaji wa majukumu yao ya kiuchumi.“tunahitaji kuendeleza amani na utulivu katika maeneo yetu, hatuwezi kufanya vizuri katika maswala ya biashara na uwekezaji kama hatuna amani na watu wetu hawawezi kufanya biashara zao wakiwa huru bila hofu”
Alihitimisha kwa kuagiza majina ya wale wote waliosomwa wakihusishwa na uhalifu kuhakikisha kuwa wameripoti katika vituo vya polisi kabla ya saa 12 jioni siku hiyo waliyotajwa majina kabla msako haujapita kokote.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa