Na, Edigar Nkilabo
Kamati ya siasa ya wilaya ya Sikonge imekagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata za Igigwa na Sikonge ikiwemo miradi ya elimu ,barabara na maji ikiwa ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020.
Akizungumza katika ziara hiyo kwa niaba ya mwenyekiti wa CCM Wilaya , Katibu wa CCM wilaya ya Sikonge SALUM MGAYA amesema ameridhishwa na usimamizi wa miradi ya elimu unaofanywa na makatibu wa kamati za ujenzi na wataalamu wa halmashauri katika shule za sekondari Sikonge na Usupilo.
“Kamati ya siasa ya wilaya tumeridhishwa na kazi inayofanywa na mafundi katika kikubwa ongezeni kasi ya ujenzi ili miradi hii ikamilike kwa wakati kama ambavyo mmeeleza katika taarifa zenu ili watoto waanze kunufaika na miradi kwa kupata elimu bora”alisema.
Kwa upande wake mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Sikonge , katibu tawala wa wilaya ya Sikonge Andrea Nghw'ani amesema serikali itafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na kamati ya siasa ili kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuwapunguzia watoto adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu huku makatibu wa kamati za ujenzi wa shule za sekondari Sikonge na Usupilo wanaelezea faida walizopata wananchi wa maeneo hayo ikiwemo ajira.
“Wananchi wengi wamejitokeza na kuomba kazi mbalimbali katika miradi hii na hata vibarua wanaofanya kazi hapa ni vijana wa humu humu Sikonge wamejipatia kipato kupitia miradi hii”
Baada ya kuipa kisogo miradi ya elimu macho yalielekezwa katika miradi ya Barabara ikiwemo ujenzi wa mitaro katika barabara za Sikonge ambapo Meneja wa TARURA wilaya ya Sikonge Elgidius Method amesema bajeti ya wilaya ya Sikonge kwa mwaka huu wa fedha ni zaidi ya milioni mia tano ambapo fedha hizo zimetumika katika ufunguzi wa Barabara,uchongaji na ukarabati wa Barabara pamoja na kuweka taa katika baadhi ya vitongoji hasa vile ambavyo tayari Barabara zake zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Ziara ya kamati ya siasa ya wilaya ya Sikonge imehitimishwa kwa kukagua mradi wa maji katika kijiji cha Wankolongo ambapo baadhi ya wajumbe wa kamati ya siasa wameelekeza kilio chao kwa mafundi wanaotekeleza mradi huo ambao wanaonekana kusuasua licha ya kuwa nje ya muda wa mkataba wa kukamilisha mradi huo.
“Mradi huu hauendi kwa kasi kwasababu fedha za mradi huu tulihamishia kwenye mradi mwingine ambao ulikuwa unatekelezwa kwa kasi lakini tayari tumeomba fedha nyingine zikija tunarejesha kwenye mradi huu ili uweze kukamilika na kuwatua kina mama ndoo kichwani kama serikali inavyosisitiza”Mhandisi Fikiri Samadi Meneja RUWASA Sikonge.
Mradi huo wa maji unagharimu zaidi ya shilingi milioni mia tisa na unatarajia kunufaisha wakazi zaidi ya elfu nane.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa