KAMATI YA FEDHA,UONGOZI NA MIPANGO IMEFANYA ZIARA YA UKAGUZI WA MIRADI YA MAENDELEO;
Tarehe 4.5.2021
_Na.Anna Kapama,_
Ukaguzi huo umefanywa na kamati hiyo katika miradi mbalimbali ikiwemo madarasa, matundu ya vyoo katika shule za msingi Ushirika,Mwanamkola na Majengo,huku Wodi tatu za Hospitali ya Wilaya ya Sikonge zikikaguliwa pia.
Katika shule ya msingi Ushirika kamati hiyo imekagua ujenzi wa Vyumba vitatu vya madarasa, ofisi ya waalimu na Matundu 5 ya vyoo, na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo. Akisoma taarifa mbele ya Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa Shule ya msingi Ushirika Mashaka Donard amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 100, huku akiishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili huo.
Katika Shule ya Msingi Mwanamkola yenye jumla ya wanafunzi 225, kamati hiyo imekagua vyumba vitatu vya madarasa, Ofisi moja na matundu 6 ya vyoo vya kisasa vyenye thamani ya shilingi Milioni 66.6. Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa ujenzi huo Katibu wa ujenzi ambae pia ni Mkuu wa shule hiyo, Bi.Happiness Jacob amesema mradi huo unatarajia kukamilika tar.15/5/2021, huku akiwashukuru Viongozi wa mradi huo, Mbunge wa Jimbo la Sikonge, Waheshimiwa madiwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji (W).
Katika shule ya msingi Majengo kamati hiyo ya Fedha,Uongozi na Mipango imekagua vyumba viwili vya madarasa, ofisi moja na matundu 7 ya vyoo vya kisasa na chumba maalumu mradi wenye thamani ya Sh.Milioni 47.7, akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa ujenzi huo Mkuu wa shule hiyo amesema mradi huo upo katika hatua ya mwisho ya ukamilishaji na utakamilika tar.15/5/2021, mkuu wa shule hiyo ameishukuru Serikali kuu kwa kutoa fedha hizo na viongozi mbalimbali waliofanikisha mradi huo.
Katika hatua nyingine kamati hiyo imekagua mradi wa ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya Wilaya ya Sikonge ambazo ni wodi ya wanaume, wodi ya wanawake na wodi ya watoto ujenzi ambao utagharimu Sh.Milioni 500 ikiwa ni fedha kutoka Serikali kuu.
Nae kaimu Mganga Mkuu Wilaya ya Sikonge Dkt.Theopister Elisa amesema mradi huo upo katika hatua za kusimamisha boma, na kuongeza kuwa unatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka 2021.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Mhe.Rashid Magope amezipongeza kamati zote za ujenzi na wasimamizi wote wa miradi hiyo ya maendeleo na kuwataka kuendelea kutunza na kulinda miradi hiyo hasa Madarasa na vyoo ili vidumu kwa Muda mrefu, kwa kuwa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ya kisasa na matundu ya vyoo,katika shule za msingi Mwanamkola, Majengo na Ushirika itasaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule hizo, kupunguza msongamano wa waalimu katika ofisi na kuboresha mazingira rafiki ya kufundishia kwa wanafunzi wakiwemo wenye ulemavu hivyo kuongeza ufaulu zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa