MKUTANO WA BARAZA LA MADIWANI ROBO YA TATU, WAFANYIKA WILAYANI SIKONGE.
Tarehe 20.5.2021
Na.Anna Kapama.
Ni mkutano wa Baraza la Madiwani ambao hufanyika kila baada ya miezi mitatu(robo) ambao hukutana na kujadili taarifa mbalimbali za maendeleo na utekelezaji wa miradi kila robo mwaka.
Akifungua Mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe.Rashid Magope amesema katika mwaka wa fedha 2020/2021, Halmashauri ilipanga kukusanya mapato ya ndani Shilingi Bilioni 3 lakini mpaka robo hii ya tatu wamefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 1.3 tu. Hivyo amewaagiza ofisi ya Mkurugenzi na watumishi wote kuongeza juhudi zaidi Katika kusimamia ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vifaa vya kielekroniki.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Siame Mathias akitoa salamu kutoka ofisi ya Katibu Tawala mkoa amesema kuwa watumishi wanapaswa kuzingatia sheria za Utawala bora na kushirikiana kwa wote ili kuhakikisha haki sawa na uwazi kwa wananchi kwa manufaa bora na ujenzi wa Taifa. Madiwani ikiwa hawaridhishwi na utendandaji wa mtumishi katika Halmashauri kufuata Sheria na hatua za kinidhamu na si kumkataa moja kwa moja pasipo kufuata taratibu zilizowekwa.
Aidha,Siame amewataka wananchi kuchangamkia fursa ya uwekezaji kwa kuwekeza hasa katika kilimo cha Korosho ambacho kitaleta tija kwa wananchi hao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge,Mhe.Peres Magiri amewataka madiwani kushirikiana na watendaji na watumishi kwa ukaribu katika ukusanyaji wa mapato,huku akiwasisitiza wananchi kushiriki katika suala la ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya ulinzi na usalama.
Mhe.Magiri amewataka wawekezaji kuja kuwekeza Sikonge kwa kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo fursa za uwekezaji wa shughuli za kiuchumi zinapatikana ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mashamba makubwa(block farming),maeneo ya kuwekeza viwanda ambayo yametengwa na Halmashauri.
Katika suala la mbio za Mwenge wa Uhuru ambao unatarajiwa kupokelewa julai 13, 2021Mkoani Tabora,Mhe.Magiri amewataka watumishi na wananchi kushirikiana kufanikisha mbio za Mwenge wa Uhuru kama ambavyo imekuwa ikifanya wakati wote kwa kuwa Sikonge imekuwa ikiongoza katika mkoa wa Tabora.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Sikonge, Anna Chambala amewasisitiza watumishi na viongozi wote wa Halmashauri kuchapa kazi na kutenda haki na usawa katika kutoa huduma kwa wakazi wa Wilaya ya Sikonge ili kutimiza ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mkutano huu wa Baraza la Madiwani umehudhuriwa na wajumbe mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora,Mkuu wa Wilaya, wakuu wa Idara mbalimbali,Waheshimiwa madiwani,viongozi wa Chama cha mapinduzi(CCM) na baadhi ya wakazi wa wilaya ya Sikonge.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa