BARAZA LA MADIWANI SIKONGE LAPITISHA BAJETI YA MWAKA 2021/2022
NA ANNA KAPAMA
2 February 2021
BARAZA la Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge limepokea na kupitisha makisio ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2021/22 ya shilingi bilioni 28.3. Mkutano wa Baraza hilo ulifanyika katika ukumbi wa chuo cha Ufundi na Maendeleo (FDC) na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya
Katika baraza hilo lililoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe. Rashid Magope ambae alisema kuwa bajeti ya mwaka ujao imepanda kwa asilimia 11.7 ukilinganisha na bajeti ya mwaka wa fedha wa 2020/21 ya shilingi bilioni 25.3.
Aidha, bajeti hiyo imejikita katika vipaumbele vya kukuza uchumi na maendeleo ya viwanda, kuimarisha miundombinu ya elimu, afya, kujenga skimu za umwagiliaji wa kilimo cha mpunga katika bonde la Kalupale,uanzishaji wa mashamba makubwa ya kilimo cha mazao ya kudumu kama vile miembe na korosho,kukamilisha sehemu ya jengo la Utawala la Halmashauri, ujenzi wa viwanda vidogo na kutatua kero za wananchi.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Peres Magiri amewataka wananchi kujiandaa na kuchangamkia fursa kutokaana na kuanzishwa kwa kiwanda cha kati cha kuchakata mazao ya nyuki pamoja na kilimo cha mashamba makubwa.
Pia aliongeza kuwa bajeti ijayo ni vema ikajikita katika uimarishaji wa kilimo cha mashamba makubwa ambayo yataweza kuzalisha mazao mengi na kupelekea kupata fedha nyingi ili asilimia 10 ya fedha hizo ikatumika kuwezesha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kuchangia miradi ya maendeleo kwa kiwango kikubwa.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka Madiwani kushirikiana na watendaji na jamii katika kuhamasisha wanafunzi wa madarasa ya mitihani kuweka kambi za maandalizi ya mitihani ya kitaifa ili kuinua ufaulu.Alisema hatua hii inakwenda sanjari na mapambano dhidi ya utoro sugu miongoni mwa wananfunzi ikiwemo kuwachukulia hatua wahusika kwa mujibu wa Sheria zilizopo. Pia alimuagiza Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Sikonge kuendesha oparesheni ya kukamata wanafunzi wote watakaokutwa wakicheza kamari na mabonanza.
Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Sikonge, Tito Luchagula aliwashukuru wajumbe wa baraza wakiwemo Madiwani na Wataalam waliohusika katika mchakato wa kuandaa na kujadili bajeti hiyo lakini pia aliwashukuru wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuhudhuria baraza hilo na kupitisha bajeti hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa