Na, Edigar Nkilabo – SikongeDC
Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge inatarajia kunufaika na mradi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) wa kuboresha miundombinu ya reli ya kati (MGR) ambao utaanza mapema mwaka huu kwaajili ya kuiongezea kasi na uwezo wa kubeba mizigo inayotoka bandarini na kupelekwa mikoa mbalimbali inayopitiwa na reli hiyo.
Akizungumza katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Sikonge wakati wa kutambulisha mradi huo, Mratibu wa Mazingira na Jamii Mha.Dkt.Veronica s. Mirambo amesema miongoni mwa Wilaya zitakazonufaika na matunda ya maboresho ya reli ya kati ni pamoja na Sikonge kwakuwa mradi huo umepita katika kijiji cha Nyahua kilichopo Wilayani Sikonge.
“TRC inapopitisha miradi yake wakazi wa maeneo husika hunufaika moja kwa moja na wengine hupata manufaa ya jumla mfano tutajenga mabwawa kwenye baadhi ya maeneo ya miradi na kuhamasisha kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ambacho hakiathiri mazingira pamoja na kuotesha nyasi kando kando ya reli”alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas M. Myinga amewashukuru TRC kwa kuutambulisha mradi huo kwa Viongozi na Wataalamu wa Halmashauri ambao watasaidia kuepusha migongano ya kiutendaji pamoja na krahisisha mahitaji ya TRC kwa serikali ya wilaya ya Sikonge.
Aidha Myinga amewasihi kwenda kutoa elimu kwa wananchi ili watambue faida watakazopata kutokana na mradi huo.
“Wananchi waelimishwe juu ya mradi wajue kuwa watapata ajira za kufanya kazi na wengine watanufaika na ule mnyororo wa thamani wa shughuli mbalimbali zinazofanywa kama vile Mamantilie, kwakupewa kwao elimu tunaamini wataulinda mradi kwa kuepuka wizi wa vifaa vya mradi”alisema Mhe.Myinga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg.Seif Salum ametoa wito kwa Wataalamu wa TRC kuzingatia masuala ya mazingira ili mradi huo usiwe chanzo cha uharibifu wa mazingira hasa maeneo ya hifadhi huku Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg.Festo Nyang’anyi akisisitiza suala la wakazi wenyeji wa eneo la mradi kupewa kipaumbele kwa kazi za vibarua ili waweze kunufaika na mradi huo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa