Na Linah Rwambali
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe.Thomas Myinga ametoa wito kwa Watumishi wa umma kuzingatia haki katika utoaji wa huduma ili kuepukana na mafarakano katika jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo maalumu kwa Watumishi walioajiriwa kati ya Januari 2023 hadi Julai 2025 yaliyofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri, Mhe.Myinga aliwasisitiza kuwa waadilifu na kuelewa sera za serikali ili wajue namna ya kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya serikali.
“Zingatieni haki katika utoaji wa huduma. Mahali pasipo na haki huleta chuki hivyo basi kila mtumishi kwa nafasi yake azingatie kutoa huduma bila upendeleo wa kidini,kikanda na kikabila , lazima uelewe wewe ni mtumishi wa wananchi wote” amesema.
“Kila mmoja asome na kuelewa sera za serikali kuhusu eneo alilosomea, hiyo itakusaidia kumwelezea mwananchi muongozo wa serikali katika Idara au Kitengo chako, pia itakusaidia wewe mtaalamu kufanya kazi kwa weledi.” amesema Mhe.Myinga.
Mbali na hayo Mhe. Myinga amewataka watumishi wote kushiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru ifikapo Julai 29. Alisema kuhudhuria tukio hilo si hiari bali ni suala la lazima.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Selemani Pandawe ametaja malengo na matarajio ya kufanyika kwa mafunzo hayo.
“Mafunzo haya yanalenga kuwawezesha watumishi kuelewa misingi ya utawala bora, kufahamu muundo wa serikali za mitaa, kufahamu sheria za uendeshaji wa serikali za mitaa, kufahamu kanuni na maadili ya utumishi wa umma na kufahamu haki na wajibu wa watumishi wa umma. Tunatarajia watumishi waliokuja katika mafunzo watapata mbinu za msingi za namna ya kutekeleza majukumu yao” amesema.
Opportuna Kalewa kutoka Kitengo Cha Ununuzi na Ugavi ni miongoni mwa Watumishi wapya waliopatiwa mafunzo maalumu anasema maarifa waliyoyapata yatawasaidia kutoa huduma bora kwa wananchi pamoja na kutunza siri za serikali.
“Kwakweli haya mafunzo yatatusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja wetu, tumejua miiko na maadili ya utumishi wa umma hivyo tutatunza siri za serikali na kuepuka migogoro baina yetu na jamii tunayoihudumia”alisema.
Mafunzo hayo yaliyohudhuriwa na wakuu wa Idara na vitengo mbalimbali pamoja na zaidi ya watumishi mia tatu toka Idara na vitengo tofauti walioajiriwa kati Januari 2023 hadi Julai 2025 yaliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) chini ya Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa