Na, Edigar Nkilabo
Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeendesha mafunzo maalum ya mfumo wa E-Utendaji(PEPMIS) kwa wasimamizi wa watumishi wa umma ili kuimarisha uwajibikaji na utendaji wa watumishi wa umma kwa kutumia mfumo huo wa kisasa.
Akizungumza katika ukumbi wa Halmashauri wakati akiwasilisha mada juu ya mfumo huo, Mwezeshaji Mfumo wa PEPMIS kutoka OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bi.Cecilia Meela amesema kuwa mafunzo hayo ni utekelezaji wa adhima ya serikali ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu kwa njia ya kidigitali unaoendana na kasi ya mabadiliko sayansi na teknolojia.
“Mafunzo haya yanalenga kuelekezana juu ya matumizi sahihi ya mfumo mzima wa e-Utendaji katika uwekaji wa taarifa za utekelezaji hasa kipengele cha tathmini ya utendaji wa watumishi.Ni wajibu wa watumishi wote kuhakikisha tunaujua huu mfumo asiwepo yeyote anayeachwa nyuma ili iwe rahisi kuweka utekelezaji na kuidhinisha kwakuwa upandishaji wa madaraja unategemea taarifa za utendaji za kwenye mfumo wa PEPMIS na si vinginevyo”alisema Bi.Meela.
Aidha Bi.Meela amewataka watumishi kuwa makini na taarifa zao kwa kutunza nywila za akaunti zao za PEPMIS kwakuwa wapo baadhi ya watu si waaminifu wanaweza kuzitumia vibaya taarifa hizo na kumletea hasara mtumishi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Sikonge Ndugu Andrea Ng’hwani amewataka Watendaji wa Kata,Wakuu wa Shule za Sekondari,Walimu wakuu wa Shule za Msingi,Waganga Wafawidhi wa Vituo vya Afya, Zahanati na Wakuu wa Idara na vitengo wote kuzingatia mafunzo hayo ili yalete tija kama ilivyokusudiwa.
“Mkitoka hapa mkatekeleze mafunzo mliyopatiwa najua hata zile changamoto za awali zitapatiwa suluhisho kupitia mafunzo haya, hakikisheni na wale waliokosa hii fursa mnawaelekeza”alisisitiza Ng’hwani.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Dkt.Christopher Nyalu ameishukuru OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kutoa mafunzo hayo ambayo yataongeza weledi na ufanisi kwa watumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu katika mfumo wa e-Utendaji.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa