WATUMISHI MSIINGIE MIKATABA NA TAASISI ZA MIKOPO ZISIZO NA MIKATABA NA HALMASHAURI" DHRO SIKONGE.
Mkuu wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu (W), NICO KAYANGE amewaasa watumishi wa Umma kutokuingia mikataba ya Mikopo na taasisi binafsi za mikopo ambazo hazitambuliwi na Halmashauri kisheria.DHRO Kayange ambae pia amemuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji(W) ameyasema hayo alipokutana na watumishi wa Umma baada ya kufanya Ziara ya kuwatembelea watumishi wa kata ya Tutuo na Mole akifanya nao mazungumzo na kuwasikiliza changamoto na kero wanazokutana nazo wakiwa katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, DHRO Kayange amebainisha miongoni mwa mambo yanayotesa watumishi ni pamoja na mikopo kutoka kwa taasisi binafsi ambazo zimekuwa na mikataba na masharti ambayo wakati mwingine yamekuwa kero kwa watumishi na kuongeza kuwa hali hiyo inapelekea watumishi kushindwa kusaidiwa na Halmashauri endapo changamoto zitawapata wakati wa ulipaji kutokana na Halmashauri kutozitambua taasisi hizo kisheria.Aidha,DHRO ametumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi wote wa Umma Wilayani hapo kufanya kazi kwa nidhamu na Weledi wakifuata sheria za utumishi huku akiwataka kuwasilisha kero na changamoto zao kwa Mkurugenzi ili zitatuliwe na si kuzipeleka mahali pasipohusika.
Sambamba na hilo,DHRO Kayange amewapongeza watumishi wakiwemo walimu na watoa huduma za Afya kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutoa huduma stahiki kwa jamii na kwamba juhudi zao zimeonekana kuleta tija kwa wananchi wa Sikonge.Katika hatua nyingine baadhi ya watumishi waliohudhuria kikao hicho wamewasilisha changamoto na kero ambazo zimekuwa zikiwakwamisha kutekeleza baadhi ya majukumu yao ikiwemo changamoto ya upungufu wa vyombo vya usafiri Kama pikipiki kwa watendaji,bwana afya na maafisa maendeleo ya jamii kero .
Naye DHRO Kayange akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji(W) ameahidi kushughulikia changamoto ambazo zimewasilishwa kwa wakati ili watumishi hao wafanye kazi katika mazingira rafiki.Mkurugenzi anaendelea na ziara katika kata zote 20 akiongozana wakuu wa Idara mbalimbali kuzungumza na watumishi wa Umma sambamba na kusikiliza changamoto zao.
Na.Anna Kapama
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa