Na Edigar Nkilabo
Watendaji wa Kata zote Wilayani Sikonge wameagizwa kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni na watoto wote wanakula chakula pindi wanapokuwa shuleni kama serikali ambayo imekuwa ikisisitiza watoto wote kupata chakula shuleni.
Agizo hilo limetolewa Katika Ukumbi wa Halmashauri na Katibu Tawala Ndg.Andrea Ng’hwani wakati akiongoza kikao cha Tathimini ya Mkataba wa Lishe kwa ngazi ya Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Sikonge ambapo amewataka Watendaji wa Kata kwenda shule moja baada ya nyingine kwaajili ya kupata taarifa sahihi za upatikanaji wa chakula shuleni na kuhakikisha watoto wote wanakula.
“Jamani hatuna haja ya kulialia kwa habari ya chakula shuleni nyie Watendaji wa Kata nendeni shule mkaangalie uhalisia wa takwimu za upatikanaji wa chakula shuleni ili wazazi wachangie lakini tusiwabane tu wazazi kuchangia chakula waoneni wadau wa maendeleo na wawekezaji katika kata zenu washirikisheni suala la chakula wawachangie”alisema.
Kwa upande wake Katibu wa Kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndugu Selemani Pandawe ametoa wito kwa Watendaji wa Kata kwenda kusimamia mapato na matumizi ya vijiji.
“Huko kwenye maeneo yenu mnamapato huru tumieni kwa mwongozo yaani msitumie zote kwa shughuli za vijiji tu, tengeni 60% ya fedha za maendeleo na matumizi mengine, kama mtazingatia hilo naamini kipo kiasi mtapata cha kuchangia kwenye chakula na sio kuelekeza fedha nyingi kwenye posho”alisema
Naye Afisa Lishe wa Wilaya ya Sikonge Bi.VeroFerdinard amesema kwa robo ya nne ya Aprili hadi June 2025 vijiji vyote 71 vya Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge vimeweza kutekeleza siku ya Afya na Lishe ya kijiji ambapo hii ni sawa na asilimia 100 ya utekelezaji wa kiashairia hicho.
Katika kikao hicho Kata 3 ambazo ni Chabutwa,Nyahua na Kilumbi zimepongezwa kwa utekelezaji mzuri wa Maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Vijiji katika Kata zao .
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa