WATENDAJI KATA WAPEWA SEMINA SIKONGE
Wananchi waaswa kusherekea sikukuu ya mwaka mpya kwa amani na utulivu bila kuvunja sheria za nchi, ili kuhakikisha usalama kwa kila raia.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya ya Sikonge mkoani Tabora Mhe. Peres Magiri katika semina kufunga mwaka 2018 iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Bi. Martha Luleka alipokuwa akizungumza na watendaji wa kata na kuwasisitiza kuyapeleka kwa wananchi wanaowaongoza.
Semina hiyo ililenga kuwawezesha watendaji wa kata kujua majukumu yao na kuyatekeleza ipasavyo ili kujenga Sikonge yenye maendeleo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi. Martha Luleka akishirikiana na baadhi ya wakuu wa idara na vitengo, pamoja na kuu ya wilaya ikiongozwa na DC Mhe. Peres Magiri.
Bi. Martha alitoa somo la ujasiliamali kwa watendaji kama njia mojawapo ya njia ya kuwapatia kipato na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwenye kata zao. Pia walitakiwa kubuni miradi itakayoleta kipato mfano mazao na hata kutumia simu zao kujifunza mambo mbali mbali ya kimaendeleo. Akitoa msisitizo alisema “kiongozi anaanzia nyumbani kwake, ili uwe kiongozi wa pekee lazima ufanye kitu cha kipekee”.
Akizungumza na watendaji Mhe. Peres amepiga marufuku kumbi za video kufanya maonesho usiku huku watoto wakiwemo ndani ya kumbi hizo, kwani jambo hilo ni kinyume cha sheria na pia wakati mwingi picha zinazooneshwa usiku katika kumbi hizo ni zile zisizo na maadili. Hivyo kuwataka watendaji wa kata kushirikiana na vyombo vya usalama kukomesha jambo hilo.
Miongoni mwa mambo aliyoyakemea Mhe. Magiri ilikuwa ni pamoja na watoto kushiriki katika mchezo wa bahati nasibu maharufu kama KUBET, kucheza Puli muda wa kazi pamoja na kufanya mikusanyiko isiyokuwa na kibali kutoka katika vyombo vinavyohusika.
Watendaji hao pia walipewa rai kuhakikisha wanatenda haki kwa wananchi wanowaongoza kwani kutokufanya hivyo ni kusababisha wananchi waichukie serikali yao, na kuongeza kuwa serikali ya awamu ya tano ni sikivu na inawajali wananchi wake wote.
Kwenye swala la kilimo mkuu wa wilaya alisisitiza wakulima kupiga dawa mapema kwenye mazao ili kuepukana na wadudu waharibifu ambao wamekuwa wakishambulia mazao yaliyoko shambani, pia wakulima na wafugaji watengewe maeneo maalumu ili kuepuka migogoro ya ardhi.
Wafugaji wamesisitizwa kupitisha mifugo yao kwenye njia zilizotengwa maalumu kwa ajili ya mifugo. kwani kupitisha mifugo kwenye barabara kuu ni kuharibu hifadhi ya barabara wakati serikali inatumia pesa nyingi kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za barabara. Hivyo wafugaji wanaokiuka kanuni hiyo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Magiri pia alizungumzia swala la elimu katika wilaya ya Sikonge na kusema kuwa inatakiwa vyumba 7 vya madarasa kuongezwa ili kukabiliana na changamoto ya watoto 361 ambapo wavulana walikuwa 126 na wasichana 235 walikosa kuchaguliwa baada ya vyumba vya madarasa kuwa vichache.
Swala la mimba mashuleni ambalo ni changamoto, awamu hii Mhe. Magiri amelivalia njuga na kusema kuwa “hatokubali kila siku watoto wanapigwa mimba na sisi tupo tunaangali tu.’’ Hivyo kila mtu ajiandae kuanzia ngazi ya familia na Watendaji watoe ripoti mapema ya kesi za mimba kwa jeshi la polisi ili zishugulikiwe mapema na sio kungojea hadi wanafunzi wanajifungua.
Watendaji hao kwa pamoja walitoa ahadi ya kuyafanyia kazi maagizo waliyopewa wao kama viongozi katika kata zao watatoa maamuzi kwa haki na kutatua changamoto ambazo zilikuwa sugu mwaka 2018. Ili kutekeleza sera Mhe. Raisi kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa