Na Edigar Nkilabo
Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge Mwl.Benjamin Mshandete amewataka Wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata kuhakikisha wanazingatia viapo vyao kwa kutunza siri na kusimamia katiba, sheria ,kanuni na miongozo inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi kipindi cha Uchaguzi Mkuu.
Mwl.Mshandete ametoa kauli hiyo katika ukumbi wa Halmashauri wakati akifungua mafunzo ya Wasimamizi wasaidizi ngazi ya kata.
“Hakikisheni viapo mlivyokula mnavizingatia pia someni katiba ya nchi, pitieni sheria,kanuni na miongozo inayotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na pale ambapo mtu hujaelewa basi uliza ili ufafanuliwe ili mkafanye kazi vizuri katika maeneo yenu wakati wa Uchaguzi mkuu kwa niaba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi” alisema.
Aidha Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge amewapongeza Wasimamizi wasaidizi wote walioaminiwa na kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuwakumbusha kuwa uteuzi wao umezingatia bidii, utendaji kazi, weledi na uzalendo wao kwa Taifa hivyo hawana budi kuwajibika ipasavyo kama walivyoaminiwa na tume.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mafunzo Bi.Fatuma Said amemshukuru Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Sikonge kwa kuwapa somo ambapo amesema kupitia mafunzo haya wataenda kufanya kazi kwa umahili na ufanisi.
“Kwakweli katika kundi letu hili wapo baadhi ya Wasimamizi wasaidizi ambao hii ndiyo mara yao ya kwanza kusimamia uchaguzi na wengine wanauzoefu hivyo tukishirikiana kwa pamoja na haya mafunzo tuliyopatiwa basi tutafanya vizuri katika maeneo yetu”alisema.
Wasimamizi wasaidizi (40) kutoka kata zote (20) za Jimbo la Uchaguzi la Sikonge wanashiriki mafunzo hayo ya siku tatu ikiwa ni maandalizi kuelekea kutekeleza majukumu kama Wasimamizi wasaidizi ngazi ya Kata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa