WANANCHI WAHIMIZWA KUCHANGIA MIRADI YA MAENDELEO KWA HIARI.
Akiendelea na ziara yake katika kata 20 za Wilaya ya Sikonge,Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe.John Palingo ameendelea na kampeni ya ujenzi wa vyumba vya madarasa kata ya Kilumbi na kuwasisitiza wananchi kuchangia ujenzi wa maboma ili waweze kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madarasa katika Shule za Msingi na sekondari huku akionyesha mfano kwa kuchangia Sh.laki moja inakayosaidia ujenzi wa madarasa hayo.
DC Palingo ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Msingi Mwamalugu huku akiwataka walimu na wananchi kuhakikisha wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari zote zilizopo kata hiyo wanapata chakula wawapo shuleni.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Kilumbi, Mhe.Mayeka Mbusa ameahidi kusimamia zoezi la upatikanaji wa chakula shuleni sambamba na kuwahamasisha wananchi kujitolea kujenga maboma ya madarasa ili serikali kupitia tozo za miamala iweze kutoa fedha za ukamilishaji wa madarasa hayo.
Mhe.Palingo ametembelea vijiji mbalimbali vikiwemo Majojoro,Kilumbi,Mwamalugu na Mtendeni akihamasisha ujenzi wa madarasa, Chanjo ya UVIKO-19,pamoja na kusikiliza kero za Wananchi sambamba na Kukagua miradi ya maendeleo.
Na.Anna Kapama.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa