Na. Robert Magaka – Sikonge.
Timu ya wataalam kutoka Mkoa wa Tabora pamoja na Wilaya ya Sikonge wametembelea kijiji cha Kipanga kuongea na wanachama wa chama cha wafugaji wa nyuki juu ya mradi wa kituo cha kukusanyia mazao ya nyuki kinachotarajiwa kujengwa hivi karibuni katika kijiji cha Kipanga kilichopo kata ya Kipanga wilayani Sikonge.
Wataalam hao ni pamoja na Bw. Nyassary Goshashy,Afisa wa Maliasili wa mradi wa BEVAC kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Bw. Jordan Kabyemela,Mhandisi toka Enabel,Bw. Daniel Bikora,Mratibu wa mradi wa BEVAC kanda ya Tabora pamoja na Afisa Nyuki Wilaya ya Sikonge Bw. Samwel Samumba.
Akiwasilisha mpango wa mradi huo Bw. Bikora amesema kituo hicho kitasaidia kutunza mazao ya nyuki kwa ustadi na ubora unaotakiwa na kusababisha thamani ya mazao hayo kutoshuka,kwani utunzaji wa mazao ya nyuki nyumbani unaweza kusababisha kupotea kwa thamani ya mazao ya nyuki na kuathiri soko lake kwa wafugaji hao.
Mradi huo utaghalimu kiasi cha shilingi Milioni 106 mpaka kukamilika.Utekelezaji wa mradi huo utazingatia ushirikishwaji wa wanachama kwa kuchangia baadhi ya gharama ikiwa ni pamoja na nguvu kazi,utoaji wa eneo litakalotumika kujenga kituo hicho,ujenzi wa choo,upatikanaji wa samani za ofisi ya kituo hicho pamoja na gharama za kuingiza umeme katika jengo hilo.
Kituo hicho cha kukusanyia mazao ya nyuki kitakwenda kuinua uchumi wa wafuga nyuki kwa kuwaunganisha moja kwa moja na mfumo wa stakabadhi ghalani na hivyo kukomesha uwepo wa walanguzi wanaofaidika peke yao na kuwaacha wafungaji katika lindi la umasikini.
Chama cha wafugaji wa nyuki “Kipanga Beekeepers” wapatao 184 wamepokea mradi huo kwa shangwe na ari ya kushiriki kikamilifu katika mradi huo huku diwani wa kata hiyo Mhe. Yuda William Mbegani akisisitiza mshikamano na kujitoa ili kufanikisha mradi huo wa kimkakati.
Wilaya ya Sikonge inakwenda kuwa mnufaika wa kwanza wa mradi huo kwa kanda ya Tabora na iwapo mradi huu utaonesha ufanisi katika biashara ya mazao ya nyuki vituo vingi zaidi vitakwenda kujengwa katika Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora na mikoa mingine ya Shinyanga na Singida.
BEVAC (The Beekeeping Value Chain Support) ni shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na mradi wa kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya nyuki Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa