Na Linah Rwambali
Zaidi ya walimu 200 wa shule za Msingi kutoka Kata mbalimbali Wilayani Sikonge wamepatiwa mafunzo ya namna ya kufundisha somo la Kiingereza kwa watoto wa darasa la kwanza.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika vituo viwili Wilayani Sikonge ambavyo ni shule ya Sekondari Kamagi na Elimu maalum yametolewa kwa lengo la kuwajengea walimu uwezo wa kufundisha somo hilo kwa usahihi haswa katika kipengele cha matamshi na hatimaye kutengeneza msingi mzuri kwa wanafunzi wa darasa la kwanza.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Afisa Mwandamizi Idara ya Msingi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi.Mbutwole Emmanuel amesema mafunzo hayo yanatolewa kwa walimu wa darasa la kwanza sababu wamegundua msingi wa somo la Kingereza kwa darasa la kwanza ni mbovu.
Aidha Bi.Mbutwole amesema wamewaita walimu wakuu katika mafunzo hayo ili wajue kile ambacho walimu wao wa lugha watafundishwa katika mafunzo hayo na kwenda kuleta mabadiliko kwa wanafunzi katika somo la kiingereza.
“Tunataka kutengeneza uelewa na ufaulu wa somo la Kingereza kwa kuwajengea watoto msingi mzuri. Tunaamini wanafunzi wa darasa la kwanza wakifundishwa vyema wataweza kuzungumza lugha ya kingereza kwa urahisi na kukomesha uwepo wa idadi ya wanafunzi wasioweza kuzungumza lugha hiyo hapo badae” amesema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndugu Nico Kayange ameishukuru wizara ya Elimu kwa mafunzo hayo na kuwataka walimu kufuatilia vyema yale watakayofundishwa.
“Fuatilieni kwa makini mafunzo mtakayopewa, ulizeni maswali mahali ambapo hamtaelewa ili muondoke na uelewa wa kutosha wa kufundisha somo la kingereza kwa watoto wa darasa la kwanza”
Naye Mwenyekiti wa mafunzo na Mwalimu wa shule ya Msingi Chabutwa ambae ni moja ya walimu waliohudhuria katika mafunzo hayo Ndugu Athumani Kalunguyu, ameishukuru serikali kwa kuwaandalia mafunzo hayo na kuahidi kwa niaba ya wenzake kuwa watakua watulivu na kusikiliza kwa makini mafunzo yote watakayopewa ili watoto wakanufaike na ujuzi watakaoupata.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI yamezinduliwa na kuanza kutolewa leo na yanatarajiwa kuhitimishwa Mei 23, ambapo hivi sasa Halmashauri saba zimeshapata mafunzo hayo kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Tabora.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa