Na Edigar Nkilabo
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndugu Selemani Pandawe amewataka Walimu kuwa waadilifu na kuzingatia maadili ya Utumishi wa umma pindi wanapotekeleza majukumu yao na kuwa mfano bora wa kuigwa katika jamii.
Akifungua mafunzo elekezi ya Utumishi wa umma kwa Walimu walioajiriwa wilayani Sikonge katika kipindi cha mwaka 2025, katika ukumbi wa Elimu maalumu Pandawe amewataka Walimu kuzingatia ujuzi na elimu watakayopewa na Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ili waweze kutumia maarifa hayo katika kulea na kuwafundisha watoto kwa uadilifu na weledi.
“Utumishi wa Umma hauna mipaka wakati wote ishi katika uadilifu haijalishi uko ndani au nje ya Ofisi hakikisha unakuwa muadilifu na kuyaishi maadili ya utumishi wa umma.”alisema.
Naye Katibu Msaidizi TSC Wilaya ya Sikonge Bi. Farida Ndyamukama amesema mafunzo haya yanalenga kukazia maadili na uadilifu katika utendaji kazi kama ambavyo serikali inasisitiza mafunzo hayo ili kuepusha masuala ya utovu wa nidhamu kwa walimu.
“Mafunzo haya tunaanza kuyatoa kwa Walimu walioajiriwa baadae tutayafanya kwa Walimu wote kwakuwa wapo walimu ambao wametekwa na mazingira na kujisahau kama wao ni Watumishi wa umma hivyo inabidi kuwapiga msasa ili waendelee kuwa waadilfu katika utendaji wao wa kazi”alisema.
Kwa upande wake Afisa Elimu Kata ya Misheni Mwalimu Leonard Mwimbe amesema mafunzo hayo yataenda kuleta mabadiliko chanya katika Wilaya ya Sikonge na kuongeza ufaulu kwakuwa Walimu watafanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia maadili na miiko ya utumishi wa umma.
“Kwakuwa tayari tumeshakuwa Walimu mahali popote tunapokuwa ni lazima kuishi kama Walimu , pia tujitahidi kutumia rasilimali za umma kwa manufaa ya umma kama ambavyo serikali inakusudia na huo ndiyo uadilifu”alisema.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2021/2022, 2022/2023 hadi 2023/2024) Walimu wapatao 12,600 kote nchini, walifukuzwa kazi na kupoteza nafasi za utumishi wa umma kwa makosa ya kimaadili na kukosa uadilifu kazini.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa