Na Edigar Nkilabo – Sikonge DC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mwl.Selemani Pandawe amewataka Wakuu wa Divisheni, Vitengo na Maafisa bajeti wote kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu pamoja na mpango mkakati wa Halmashauri ambao utasaidia bajeti zao kuakisi mahitaji halisi ya Halmashauri na serikali kwa ujumla.
Mwl.Pandawe amesema hayo katika ukumbi wa Halmashauri wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa wakuu hao wa divisheni na vitengo pamoja na Maafisa bajeti.
“Mafunzo mnayopatiwa leo mnapaswa kuyazingatia kwa makini maana wakati wa bajeti mnatakiwa kuutumia ujuzi mnaopewa hapa pamoja na maelekezo yote ya wataalamu bila kusahau mpango mkakati wa Halmashauri yetu ya Sikonge ili bajeti zenu ziweze kutekelezeka na kuakisi mahitaji halisi ya Idara na Vitengo vyenu” alisema.
“Mkawashirikishe Watumishi waliopo chini ya Idara na Vitengo vyenu wakati wa uandaaji wa bajeti ili na wao watoe maoni yao, naamini mkifanya hivyo zitaandaliwa bajeti zinazokidhi mahitaji na kutatua changamoto zenu”aliongeza.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Mwl.Pandawe amewataka Wakuu wa Divisheni na Vitengo kukaa pamoja na Watumishi waliopo chini ya Ofisi zao na kubangua bongo ili kuja na vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri yatakayowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Kwaupande wake Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu Ndg.Aidan Frument amesema maagizo yote yaliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji yatafanyiwa kazi na matokeo chanya yatapatikana kwa kuhakikisha washiriki wote wa mafunzo wanazingatia hayo wakati wa uandaaji wa bajeti.
“Nyote mmesikia haya tunayoelekeza myazingatie ili wakati wa bajeti kusitokee changamoto zaidi tupange kwa kuzingatia mpango mkakati wetu, dira ya taifa pamoja na ilani ya chama tawala hapo tutakuwa ndani ya malengo ya serikali na bajeti zetu zitaendana na mahitaji”alisema Ndg.Frument.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanalenga kujengeana uwezo wa kuandaa mipango na bajeti zinazoendana na mikakati ya Halmashauri pamoja na serikali kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa