MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan amewataka wafanyabiashara wadogo kulipia na kuchukua vitambulisho maalumu vilivyotolewa na Serikali kwa ajili yao vinginevyo watahesabika kuwa ni wafanyabiashara wakubwa wanaopaswa kulipia kodi.
Hatua itasaidia kuwatambua na kuepusha usumbufu wakati wa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo.
Makamu wa Rais alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa TASAF wilayani Sikonge ikiwa ni siku tatu ya ziara yake mkoani Tabora .
Alisema mfanyabiashara ndogo ndogo asiyetaka kulipia shilingi 20,000/- za kitambulisho maalumu atahesabika kuwa yeye anapaswa kukata leseni na kulipa kodi kama walivyo wafanyabiashara wakubwa.
Makamu wa Rais aliongeza kuwa kama shilingi 20,000/- zinaonekana ni nyingi kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo kulipa kwa mkupuo, uongozi wa Mkoa, Wilaya unaweza kuweka utaratibu ambao utawawezesha kulipa kwa awamu.
Alisema mfanyabiashara huyo anaweza kulipa kwa awamu mbili au tatu na akishamaliza malipo anakabidhiwa kitambulisho chake.
Ili kutambua mchango wa wafanyabiashara wadogo mama Samia pia alitoa hundi ya shilingi ml.40 kama mkopo kwa vikundi 40 vya wajasiliamali ambazo zimetokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya Sikonge huku akisisitiza kuwa wazitumie kujikwamua kiuchumi.
Aidha Makamu wa Rais alitoa angalizo kwa viongozi wa Mamlaka ya Mikoa na Serikali za Mitaa kuhakikisha hakuna Mfanyabiashara atakayepewa kitambulisho kabla ya kumaliza malipo yote kuwa upo uwezekano wa kutoroka na kwenda Mkoa mwingine na kuendesha shughuli zake kwa kutumia kitambulisho ambacho bado anadaiwa.
Awali Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Mhe. Joseph Kakunda alisema Serikali imesikia kilio cha wafanyabaishara ndogo ndogo na itashughulikia matatizo yaliyojitokeza wakati wa uchukuaji vitambulisho .
Akiwa katika ziara yake wilayani humo mama Samia pia alishiriki kupanda miti katika jingo la ofisi za Halmashauri ikiwa ni jitihada za kuunga mkono utunzaji wa mazingira ambapo alisisitiza wakulima wa tumbaku kutumia tekinolojia ya sola na umeme kwaajili ya kukaushia mazao yao ili kuendelea kuhifadhi mazingira.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa