Kikao cha kujadili maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa kimefanyika wilayani Sikonge, kikijumuisha wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi za umma, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wawakilishi wa makundi maalum, ikiwemo wanawake na vijana.
Akizungumza katika kikao hicho, msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Sikonge, Ndg. Seleman Pandawe, amesisitiza umuhimu wa kufuata sheria na kanuni za uchaguzi, na kujengeana uelewa miongoni mwa wadau kuhusu masuala mbalimbali yaliyoibuka katika mjadala wa kikao hicho.
“Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa utazingatia falsafa ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya 4R, ambayo ni Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko, na Kujenga Upya,” alisema Ndg. Pandawe. Aliongeza kwamba, “Hatutaruhusu uwepo wa taharuki, vurugu, au ukakasi wa aina yoyote ile ; tupo tayari kumsaidia mwanachama au mgombea yeyote atakayekumbana na changamoto katika ujazaji wa fomu za uchaguzi.”
Kwa upande wao wadau wamefurahishwa na kikao hicho, wakiahidi kuwa mabalozi wema katika maeneo yao kwa kufikisha maarifa na taarifa sahihi kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa. Pia wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwajengea wananchi utayari na uelewa wa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.
Kikao hiki ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa amani na utulivu, huku ikihakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kushiriki katika mchakato huo muhimu.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa