VITAMBULISHO VYAMSUKUMA NDANI MTENDAJI KATA.
MKUU wa Mkoa amuweka ndani Mtendaji wa kata ya Kitunda Bwana Jerad Hamis Kwa tuhuma za kuuza vitambulisho vya wajasiliamali wadogowadogo kwa shilingi elfu 26.
Hatua hiyo ilichukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Agrey Mwanri alipozungumza na wananchi kutaka kujua nini kinachokwamisha zoezi la uuzwaji wa vitambulisho hivyo ambapo wajasiliamali hao walilalamikia kuuziwa kwa shilingi elfu 21 mpaka elfu 26.
Mtendaji huyo aliwauzia wakazi wa kitunda Mgodini vitambulisho kwa bei tofauti na bei iliyopangwa na Serikali ambayo iliagiza kitambulisho kimoja kichangiwe shilingi elfu 20 tu ambazo ni gharama za utengenezaji na si vinginevyo.
Akilaani kitendo hiko Mwanri alisema kuwa hakuna mahali kamati ya ulinzi na usalama ilikaa na kupitisha zaidi ya pesa iliyowekwa na serikali hivyo maagizo ya mtendaji huyo hayajulikani yalipotokea. Aliongeza kuwa pesa zote za ziada zilizotozwa zirudishwe kwa wananchi na Mtendaji huyo awajibishwe, aliongeza kwa kusema “amepoteza sifa ya kuwa mtumishi kwani anaichanganya Kadamnasi”
Pia alitoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge kufuatilia jambo hilo kwa kwa ukaribu ili haki itendeke na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria ya nchi huku akitoa onyo kwa jeshi la Polisi kutoivuruga kesi hiyo kwani ina maslai mapana ya nchi ya Tanzania.
Akipokeaa agizo la hilo Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Mhe. Peres Magiri alisema kuwa tukio hilo linasikitisha sana na halikubaliki hata kidogo na kusisitiza kuwa pesa zote zitarudishwa kwa wahusika huku akiitaka Kuu ya Wilaya kuhakikisha wote walioshiriki wanachukuliwa hatua wakati huohuo alihaidi kutekeleza maagizo yaote kama yalivyotolewa na mkuu wa Mkoa huku akitumia nafasi hiyo kuwatahadhalisha watumishi wengine kutojaribu mchezo huo na wananchi waliombwa kuwa na subra wakati utaratibu ukiwekwa vizuri.
Wakazi wa Sikonge wakijipanga kununua vitambulisho vya wajasiliamali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Sikonge Bi. Martha Luleka alilaani vikali kitendo hicho kwa kusema kuwa ni tukio la aibu lisilokubalika kwani mbali na kuwakera wao kama viongozi pia limewakera wananchi. Hivyo basi kwa kufuata taratibu za kiutendaji mtuhumiwa huyo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu ikiwemo kueleza alipopata maelekezo hayo na kubainisha wafuasi ambao amekuwa akishirikiana nao kufanya tendo la namana hiyo.
Akitolea ufafanuzi wa namna alivyokusanya pesa zaidi ya kiasi kilichobainishwa na Serikali, Mtendaji Bwana Jerad alisema kuwa kiasi kilichotozwa kilikuwa ni shilingi elfu ishirini na gharama ya shilingi elfu moja ilitokwa ili kutolea nakala ya kitambulisho huku elfu 5 ilitozwa kama faini kwa watu walioleta ubishi ikiwemo lugha ya kashfa hivyo kupelekea jumla ya gharama kufikia shilingi elfu ishirini na sita.
Mkuu wa mkoa alifanya ziara ya kuhamasisha wajasiliamali wadogo wadogo katika kata ya Kitunda na Kipili zilizoko Wilayani Sikonge Mkoani Tabora, ambapo alitoa semina kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwa na vitambulisho hivyo kwani ni njia pekee ya wananchi kuepukana na bugdha katika biashara zao. Sababu ikiwa ni kutambuliwa na serikali na kuwekewa utaratibu mzuri ikiwemo maeneo ya kufanyia biashara.
Wananchi wengi walipokea kwa muitikio mkubwa sanjari na kununua vitambulisho hivyo maalufu kama Viparata huku wasio kuwa na pesa wakijiorodhesha majina yao ili kuanza utaratibu wa kulipa kidogokidogo na watakapokamilisha waweze kupatiwa Vitambulisho vyao rasmi.
IMETOLEWA NA
KITENGO CHA TEKINOLIJIA HABARI NA MAWASILIANO (TEHAMA)
SIKONGE.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa