Na, Edigar Nkilabo
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini REA wametoa mitungi ya gesi ya ruzuku zaidi ya 3000 kwa wakazi wa wilaya ya Sikonge ili kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda afya zao pamoja na kutunza mazingira.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Bwenge Mwesigwa wakati akizindua zoezi la usambazaji na uuzaji wa mitungi hiyo ya ruzuku ya kampuni ya Oryx gesi ambayo itauzwa kwa bei ya shilingi 20,000/= kwa wananchi wote wa vijiji vyote vya wilaya ya Sikonge.
Aidha Bwenge, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuhimiza matumizi ya nishati safi kwa vitendo na kuwataka wananchi wote kuandaa vitambulisho vyao vya Taifa au namba ya NIDA na shilingi elfu ishirini kwa ajili ya kulipia mitungi hiyo ya ruzuku ili wapate nishati safi ambayo inafaida nyingi ikiwemo kulinda afya na kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na utafutaji wa nishati ya kuni na mkaa.
Kwa upande wake Meneja wa Kanda Oryx gesi Leon Isaac amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na mwamko wa Wananchi uko juu hivyo mitungi yote itawafikia mahali walipo ili kufikia lengo la serikali la kutaka wananchi wote kutumia nishati safi.
Naye Mratibu wa Nishati safi wilaya ya Sikonge Mahuna Mahuna amesema wameandaa utaratibu mzuri wa kuzifikia kata zote na vijiji vyote vya Sikonge na kutangaza matangazo ili wananchi wote wapate huduma hiyo.
Baadhi ya wananchi wameishukuru serikali kupitia REA kwa kupata huduma ya nishati safi kwa bei nafuu hali inayowapunguzia ukali wa maisha pamoja na kuwawezesha kulinda afya zao kwa kuepuka athari za nishati chafu kama kuni na mkaa.
Lengo la serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha ifikapo 2034, wananchi wawewanatumia nishati safi ya kupikia kwa 80%.
Mkurugenzi Mtendaji Sikonge DC
Anuani ya Posta: S.L.P 70 Sikonge, Tabora
Simu: 0767135460
Simu: 0767135460
Barua pepe: ded@sikongedc.go.tz
Hatimiliki ©2017Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Haki zote zimehifadhiwa